• HABARI MPYA

  Friday, November 17, 2017

  LYANGA: NINA UWEZO WA KUISAIDIA STARS , NAHESHIMU UTEUZI WA KOCHA MAYANGA

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  WINGA wa Fanja ya Oman, Daniel Lyanga amesema kwamba anaamini ana uwezo wa kuchezea timu ya taifa ya Tanzania, lakini anaheshimu maamuzi ya kocha wa Salum Shaaban Mayanga.
  Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu kutoka Muscat, Oman jana, Lyanga alisema kwamba anaamini wakati utafika naye ataitwa kutoa mchango wake Taifa Stars. 
  “Hayo ni maamuzi ya kocha, maana yeye ndiye anachagua na anaona wapi panamfaa nani na wapi panamfaa nani. Na mimi sina tatizo na hilo, kwa kuwa wanaoitwa pia ni wachezaji kama mim na mimi itafika tu zamu yangu kama itatokea nafasi ya kuitumikia Taifa Stars nitaitwa kuitumikia,”amesema.
  Daniel Lyanga akishangilia baada ya kufunga moja ya mabao yake Fanja
  Daniel Lyanga (katikati) akishangilia na wenzake baada ya kufunga Fanja 
  Daniel Lyanga (kulia) akiwa na Mbuyu Twite (kushoto) katika moja ya safari ya mechi za ugenini za Fanja

  Lyanga ni kiungo mshambuliaji tegemeo wa Fanja kwa sasa ambaye alijiunga na timu hiyo ya Muscat Septemba mwaka jana akitokea Simba SC ya Dar es Salaam, ambayo nayo ilimrudisha nyumbani Tanzania kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alipokuwa akichezea Daring Club Motema Pembe (DCMP) ya Kinshasa mwaka 2015.
  Tangu Septemba mwaka jana, Lyanga aliyekwenda Kongo akitokea Coastal Union ya Tanga, amecheza  mechi 26 na kufunga mabao saba, huku akiseti mabao 12 kwa krosi zake maridadi.
  “Huku ninacheza sana winga zote mbili, kushoto na kulia ndiyo wananitumia sana japo msimu wa mwaka jana nilicheza namba zote za mbele hapo,”amesema.
  Katika klabu hiyo, Lyanga anacheza pamoja nyota wengine wawili aliowahi kucheza nao Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, viungo Mkongo Mbuyu Twite aliyekuwa Yanga na Muivory Coast, Kipre Michael Balou aliyekuwa Azam FC, ambao wote wanaweza kucheza kama walinzi pia.
  “Nipo nao wote huku na wote tunamshukuru Mungu tupo kama wachezaji muhimu kwenye timu, tunafurahia maisha,”amesema. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: LYANGA: NINA UWEZO WA KUISAIDIA STARS , NAHESHIMU UTEUZI WA KOCHA MAYANGA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top