• HABARI MPYA

    Tuesday, November 21, 2017

    KOCHA STARS ASEMA; “MIMECHAGUA WACHEZAJI WENYE NJAA YA MAFANIKIO”

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    KOCHA Mkuu wa Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Stars’, Ammy Conrad Ninje amesema kwamba amechukua wachezaji wenye njaa ya mafanikio kwa ajili ya michuano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge.
    Mwishoni mwa wiki iliyopita, Ninje alitaja kikosi cha wachezaji 20 kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Challnge mwaka huu nchini Kenya na leo amesema uteuzi wake ulizingatia mambo matatu.
    “Kwanza nataka mchezaji ambaye ana njaa ya mafanikio. Sehemu pekee ya kupata mafanikio ni pamoja na kucheza timu ya taifa. Pili, nataka wchezaji wanaofundishika na tatu nataka wachezaji wanaokubali kufundishwa,” amesema Ninje, Kocha mwenye leseni Daraja ‘A’ ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA).
    Ibrahim Ajib (kushoto) mmoja wa wachezaji walioteuliwa Kilimanjaro Stars akimsikiliza kocha wa klabu yake, Mzambia George Lwandamina (kulia) 
    Kikosi hicho kinachotarajiwa kuingia kambini Jumapili Novemba 26, mwaka huu jijini Dar es Salaam kina makipa Aishi Manula (Simba SC) na Peter Manyika (Singida United).
    Mabeki ni Gardiel Michael, Kelvin Yondani ( Yanga SC), Kennedy Juma (Singida United), Erasto Nyoni na Mohammed Hussein (Simba SC).
    Viungo ni Himid Mao ambaye pia ni Nahodha (Azam FC), Jonas Mkude, Muzamil Yassin, Shizza Kichuya (Simba SC), Hamisi Abdallah (Sony Sugar/Kenya), Abdul Hilal (Tusker/Kenya), Ibrahim Ajib na Raphael Daud wote Yanga SC, wakati washambuliaji ni Mbaraka Yussuph (Azam FC), Elias Maguri (Dhofar/Mascat, Oman), Daniel Lyanga (Fanja FC/Mascat) na Yohana Mkomola (Ngorongoro Heroes). 
    Benchi la Ufundi linaundwa na yeye Ninje ambaye ni Kocha Mkuu, Fulgence Novatus (Kocha Msaidizi), Patrick Mwangata (Kocha wa Makipa), Danny Msangi (Meneja), Dkt. Richard Yomba (Daktari wa timu), Dkt. Gilbert Kigadye (Daktari wa Viungo) na Ally Ruvu (Mtunza Vifaa). 
    Katika michuano hiyo inayotarajiwa kuanza Desemba 3, mwaka huu, Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi ‘A’ pamoja wenyeji Kenya, Rwanda na Libya ambayo ni timu mwalikwa kutoka Kaskazini mwa Afrika.
    Kilimanjaro Stars ambayo imewahi kutwaa mara tatu taji hilo la Challenge 1975, 1994 na 2010 tangu kuanzishwa kwake, itaaza kampeni za kurudisha heshima yake dhidi ya Libya katika kundi hilo la A utaofanyika Desemba 3, mwaka huu.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KOCHA STARS ASEMA; “MIMECHAGUA WACHEZAJI WENYE NJAA YA MAFANIKIO” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top