• HABARI MPYA

  Friday, November 17, 2017

  KOCHA PRISONS ASEMA; “SIMBA SIYO TIMU KUBWA, TUTAONYESHANA KAZI UWANJANI KESHO”

  Na David Nyembe, MBEYA
  KOCHA wa Tanzania Prisons, Mohammed Abdalah amesema kwamba Simba siyo timu kubwa, bali ni timu kongwe na haiwatishi chochote kuelekea mchezo wa kesho.
  Tanzania Prisons watakuwa wenyeji wa Simba kesho Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
  Na kuelekea mchezo huo, kocha Mzanzibari wa timu hiyo, Abdallah amesema kwamba lengo lao ni kushinda na kurudia kile walichokifanya msimu uliopita dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi walipowachapa 2-1 Uwanja wa Sokoine.
  “Tumejipanga vya kutosha kuchukua pointi tatu katika mchezo wetu dhidi ya Simba, ningependa tuondoshe hayo mawazo eti tunacheza na timu kubwa, sisi tunajua tunacheza na timu kongwe. Simba wao watakuwa na wachezaji 11, na sisi tutakuwa na wachezaji 11.  Kila mwalimu kaandaa mbinu zake, tutapambana uwanjani,”amesema.
  Kocha wa Prisons, Mohammed Abdallah (kulia) akiwa na wasaidizi wake katika mchezo wa msimu uliopita Uwanja wa Taifa ambao alifungwa 1-0 
  Mohammed Abdallah (kulia) akisalimiana na kocha wa Simba, Joseph Omog. Kila mtu alishinda nyumbani msimu uliopita

  Abdallah amesema kikosi chake kipo vizuri na hakina majeruhi hata mmoja, baada ya kambi yao ya wiki moja a ushei Kahama na Iringa, wakitokea mkoani Kagera, ambako Novemba 4 walitoa sare ya 1-1 na wenyeji, Kagera Sugar uwanja wa Kaitaba katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu.
  Amesema katika kambi yao ya siku nne Kahama walipata pia na mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya Kabela City uliomalizika kwa sare ya 1-1 Alhamisi iliyopita kabla ya kwenda Iringa, ambako wanaondokea kuingia Mbeya kwa ajili ya mchezo na Simba kesho.
  Kwa ujumla baada ya mapumziko ya kupisha mechi za kirafiki za kimataifa zikiwemo za kufuzu Kombe la Dunia, Ligi Kuu inarejea jioni ya leo kwa mchezo mmoja tu, Singida United wakiikaribisha Lipuli ya Iringa Uwanja wa Namfua.
  Mechi nyingine za Jumamosi, Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Ndanda FC Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani, Stand United na Mwadui FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Maji Maji na Mbao FC Uwanja wa Maji Maji mjini Songea na Simba SC dhidi ya Tanzania Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
  Mzunguko wa 10 utakamilishwa kwa michezo miwili, Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, Yanga watakuwa wenyeji wa Mbeya City na Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, wenyeji Njombe Mji FC wataikaribisha Azam FC.
  Simba inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 19, sawa na Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa kuzidiwa wastani wa mabao, wakati Yanga inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 17, sawa na Mtibwa Sugar.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KOCHA PRISONS ASEMA; “SIMBA SIYO TIMU KUBWA, TUTAONYESHANA KAZI UWANJANI KESHO” Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top