• HABARI MPYA

    Wednesday, November 15, 2017

    HATUA NYINGINE MOJA MBELE…SAMATTA AACHA FIMBO NA KUTEMBEA MWENYEWE KIDOGO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    HATUA nyingine moja mbele katika kupambana na maumivu yake ya goti, mshambuliaji Mbwana Ally Samatta leo amejaribu kuziacha fimbo zake maalum za kutembelea na kutembea kwa hatua kadhaa.  
    Katika siku ya tano tangu afanyiwe upasuaji mdogo wa goti, Nahodha wa Tanzania, Samatta amezidi kuonyesha matumaini baada ya jana kuanza maozezi mepesi ya gym.
    Akizunguma na Bin Zubeiry Sports – Online leo kutoka Genk, Samatta amesema kwamba anaendelea vizuri na goti lake kiasi kwamba anaweza kuanza kujaribu kutembea bila fimbo.
    Mbwana Samatta akitembea bila fimbo leo nyumbani kwake mjini Genk, Ubelgiji 

    “Naanza kuhisi nafuu mapema sana, leo nimejaribu kuziacha nyuma kwa sekunde kadhaa fimbo na kutembea,”amesema Samatta aliyefanyiwa upasuaji wa goti hilo Novemba 10 mjini Genk, Ubelgiji.
    Samatta anaelekea kumaliza wiki ya kwanza kati ya sita za mapumziko kufuatia kuumia Novemba 4, mwaka huu akiichezea klabu yake, KRC ikilazimishwa sare ya 0-0 Jumamosi na Lokeren katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Na baada ya kufanyiwa vipimo ikagundulika Samatta ameumia kwenye mishipa midogo ya goti lake la mguu wa kulia ambayo ilichanika, hivyo kuhitaji kufanyiwa upasuaji mdogo ili apone sawia.
    Samatta aliumia akiichezea mechi ya 70 Genk tangu alipojiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Na katika mechi hizo 70, Samatta, mshambuliaji wa zamani wa Mbagala Market, African Lyon na Simba za Tanzania, amefunga mabao 22 kwenye mashindano yote.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HATUA NYINGINE MOJA MBELE…SAMATTA AACHA FIMBO NA KUTEMBEA MWENYEWE KIDOGO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top