• HABARI MPYA

  Sunday, November 12, 2017

  HAKI HAITENDEKI NDANI WALA NJE YA UWANJA, SOKA YETU ITAENDELEA VIPI?

  SENEGAL imefuzu fainali za kombe la Dunia mwakani nchini Urusi baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wenyeji, Afrika Kusini Uwanja wa Peter Mokaba mjini Polokwane juzi.
  Mabao ya Senegal yalifungwa na mshambuliaji wa West Ham, Diafra Sakho dakika ya 12 na Thamsanqa Mkhize aliyejifunga dakika ya 38.
  Ikumbukwe huo ulikuwa mchezo wa marudio, baada ya ushindi wa 2-1 wa Bafana Bafana Novemba 12 mwaka jana kutenguliwa na kuamriwa mechi irudiwe, kufuatia refa Joseph Lamptey kufungiwa maisha na Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA). 
  FIFA ilimkuta na hatia Lamptey ya kupanga matokeo ili kuibeba Afrika Kusini.
  Ikumbukwe Septemba 7, mwaka huu, Idara ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2018 ya FIFA, iliagiza mchezo kati ya Afrika Kusini na Senegal uliofanyika Novemba 12, mwaka 2016 urudiwe. 
  Bafana Bafana iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi y Simba wa Teranga Novemba mwaka jana, lakini ikabainika walimtumia refa kupanga ushindi huo.
  Uamuzi huo unafuatia uthibitisho wa Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) kuafiki kifungo cha maisha cha refa Joseph Lamptey wa Ghana kwa kuvurunda kimaamuzi katika mchezo huo, hivyo kuadhibiwa na Kamati ya Nidhamu ya FIFA kabla ya kukata Rufaa iliyodunda Kamati ya Rufaa. 
  Na baada ya mchezo huo kurudiwa juzi, Senegal wanafuzu Kombe la Dunia, nafasi ambayo waliipata kuipigania haki yao nje ya Uwanja. 
  Huo ndiyo uzuri wa taratibu kufuatwa na haki kutendeka katika jambo lolote – vitu ambavyo tunavikosa katika soka ya Tanzania.
  Huku kwetu ukishaumia uwanjani hauna sehemu nyingine ya kwenda kudai na kupata haki yao – matokeo yake viongozi wanaamua kumalizia jazba zao kwenye vyombo vya Habari.
  Tangu Ligi Kuu ya nchi hii imeanza haijawahi kutokea mchezo hata mmoja ukarudiwa kwa sababu ya makosa ya kiuchezeshaji ya marefa, wakati inafahamika waamuzi wa nchi hii pamoja na kwamba hawana ubora huo, pia wanatiliwa shaka mno ya rushwa.
  Wiki mbili zilizopita, viongozi wa klabu mbili mfululizo walijitokeza kwenye vyombo vya Habari kulalamikia uchezeshaji wa marefa wakitoa na ushahidi wa maamuzi yenyewe ya kimakosa.
  Msemaji wa Simba, Hajji Sunday Manara aliwaonyesha Waandishi wa Habari video ya mechi yao dhidi ya Yanga Oktoba 28, mwaka huu Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam refa Heri Sasii akiwanyima penalti mbili za wazi.
  Wiki iliyofuata, Mtendaji Mkuu wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe akalalamikia refa Ahmed Kikumbo kuwapa bao la offside Simba katika mechi ya Novemba 5, mwaka huu Uwanja wa Sokoine, Mbeya.   
  Hawa ni viongozi waliopata uthubutu wa kulalamika pamoja na kuwapo vitisho vya wenye mamlaka kufungia viongozi wanaokwenda kinyume na kanuni zilizowekwa – lakini je wangapi ambao wanakosa ujasiri huo?
  Tunataka ushahidi wa moja kwa moja refa anachukua rushwa kwa kiongozi wa klabu ili kupanga matokeo ndiyo tuchukue hatua, tutasubiri sana!
  FIFA imemkuta Joseph Lamptey na hatia ya kupanga matokeo Afrika Kusini ishinde dhidi ya Senegal, lakini katika ushahidi ilionao hawana kitu kinachoonyesha refa huyo wa Ghana akipokea rushwa.
  Nchini Tanzania, refa mmoja anatoa maamuzi ya utata mfululizo yanayoisaidia timu ile ile mara zote na bado hatua hazichukuliwi, halafu wananchi wake wanajiuliza pembeni kwa nini soka yao haiendelei. Na kwa nini iendelee ikiwa haki haitendeki ndani na nje ya Uwanja? 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: HAKI HAITENDEKI NDANI WALA NJE YA UWANJA, SOKA YETU ITAENDELEA VIPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top