• HABARI MPYA

    Thursday, November 16, 2017

    CAF YAZIFUNGIA, GABON NA DJIBOUTI, RATIBA CHAN 2018 KESHO

    SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limezifungia Gabon na Djibouti kushiriki michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) inayohusisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee kwa kosa la kujitoa katikati ya kampeni za kuwania tiketi ya michuano ya mwakani nchini Morocco.
    Kwa kutumia kanuni ya 59 ya ya michuano ya CHAN, Kamati ya Mashindano hayo imezifungia nchi hizo katika kikao chake kilichofanyika jana mjini Rabat zisishiriki kampeni za mwaka 2020.
    Siku chache kabla ya mechi yake ya kufuzu dhidi ya Equatorial Guinea, Agosti 5, mwaka huu, Shirikisho la Soka Gabon liliwasilisha barua ya kujitoa kwenye mashindano.
    Kwa upande mwingine, Shirikisho la Soka Djibouti pia lilitoa taarifa ya kujitoa Julai 17, mwaka 2017.
    Kanuni ya 59 inasema: “Chama chochote kinachojitoa wakati mashindano yameanza kitatozwa faini ya dola za Kimarekani 10,000 na pia hakitaruhusiwa kushiriki fainali za michuano itakayofuata ya CHAN”.
    Kwa kujitoa baada ya kucheza mechi ya kwanza dhidi ya Ethiopia, kuna hatua zaidi kwa Djibouti kwa mujibu wa kanuni ya 62 ambayo inasema: “Timu yoyote ambayo inajitoa au kughairi kucheza mechi ya marudiano baada ya kucheza mechi ya kwanza nyumbani kwake, lazima irudishe gharama ya timu wageni kusafiri kwenda kwao kiasi cha dola 10,000”.
    Kwa sababu hiyo, Kamati ya Maandalizi ya mashindano hayo imelitaka Shirikisho la Soka Djibouti kulilipa Shirikisho la Soka Ethiopia dola za Kimarekani 10,000.
    Katika kikao cha jana, Kamati pia imepanga droo na ratiba ya mashindano ifanyike Ijumaa Sofitel mjini Rabat baada ya kukamilika kwa timu 16 za kushiriki mashindano hayo, kufuatia Rwanda kufuzu ikiitoa Ethiopia katika mechi ya mwishi ya mchujo.
    Timu zilizofuzu ni pamoja na wenyeji, Morocco, Angola, Ivory Coast, Libya, Cameroon, Guinea, Nigeria, Zambia, Kongo, Uganda, Rwanda, Sudan, Burkina Faso, Equatorial Guinea, Mauritania na Namibia.
    Kamati pia imethibitisha michuano itaanza Januari 13 hadi Februari 4 mwak 2018 katika miji ya Casablanca (Kundi A), Marrakech (Kundi B), Tangier (Kundi C) na Agadir (Kundi D). 
    Mechi ya ufunguzi na fainali zitafanyika kwenye Uwanja wa Mohamed V Complex mjini Casablanca, ambao pia ulitumika kwenye mchezo wa marudiano wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2017.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: CAF YAZIFUNGIA, GABON NA DJIBOUTI, RATIBA CHAN 2018 KESHO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top