• HABARI MPYA

  Sunday, November 19, 2017

  AZAM FC YAONYESHA IMEDHAMIRIA, MTIBWA SUGAR YAANZA KUJITOA MBIO ZA UBINGWA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  USHINDI wa 1-0 dhidi ya Njombe Mji FC, unaashiria Azam FC imedhamiria kweli kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu.
  Azam FC imeibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Njombe Mji FC leo Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe, bao pekee la Nahodha, Aggrey Morris kwa penalti dakika ya 60 baada ya winga Mghana, Enock Atta Agyei kuangushwa kwenye boksi.
  Azam FC sasa inafikisha pointi 22, sawa na Simba SC lakini inaendelea kukamata nafasi ya pili kutokana na kuzidiwa na wastani wa mabao (GD) na Wekundu wa Msimbazi.

  Aggrey Morris amefunga kwa penalti leo Azam ikiilaza 1-0 Njombe Mji FC 

  Wote, Azam FC na Simba wanawazidi kwa pointi mbili mabingwa watetezi, Yanga SC baada a raundi 10 za Ligi Kuu msimu huu.
  Mtibwa Sugar waliouanza msimu vizuri na kuongoza kwa takriban raundi tano, leo wameanza kujitoa taratibu kwenye mbio za ubingwa baada ya kichapo cha 1-0 kutoka kwa ndugu zao, Kagera Sugar Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.
  Bao pekee la Kagera Sugar limefungwa na kiungo mshambuliaji Edward Christopher Shijja dakika ya 84 kwa penalti, baada ya beki Dickson Daudi Mbeikya kuunawa mpira uliopigwa na Jafar Kibaya.
  Mtibwa sasa wanabaki na pointi zao 17 baada ya mechi 10, wakati Kagera Sugar iliyoanza vibaya inajivuta juu hadi nafasi ya 10, ikifikisha pointi 10 sawa na Ndanda FC baada ya mechi 10 pia.
  Njombe Mji FC inabaki na pointi zake saba katika nafasi ya 15 kwenye Ligi Kuu ya timu 16, mbele ya Stand United yenye pointi sita, nyuma ya Ruvu Shooting yenye point inane, sawa na Mbao FC na Mwadui FC yenye pointi tisa. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: AZAM FC YAONYESHA IMEDHAMIRIA, MTIBWA SUGAR YAANZA KUJITOA MBIO ZA UBINGWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top