• HABARI MPYA

    Friday, October 20, 2017

    SIMBA SC KUTIMKIA ZENJI BAADA YA MECHI NA NJOMBE KWENDA KUIFANYIA ‘MAARIFA’ YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC itaingia kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji kesho Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam na baada ya hapo itakwenda visiwani Zanzibar kuweka kambi ya kujiandaa na mahasimu, Yanga Oktoba 28.
    Kikosi cha Simba SC kikiongezewa nguvu na Kocha mpya Msaidizi, Mrundi Masudi Juma aliyechukua nafasi ya Mganda, Jackson Mayanja leo kimefanya mazoezi yake ya mwisho Uwanja wa Gymkhana mjini Dar es Salaam kuelekea mchezo wa kesho. 
    Simba inataka kushinda kesho mbele ya Njombe Mji iliyopanda Ligi Kuu msimu huu ili kupoza hasira za mashabiki wake, baada ya sare ya 1-1 Jumapili iliyopita dhidi ya Mtibwa Suhar Uwanja wa Uhuru pia.
    Nahodha Msaidizi wa Kikosi cha Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ ambaye amekuwa nje tangu kuanza kwa msimu huu kutokana na maumivu sasa yuko fiti kurudi uwanjani.
    Tshabalala amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba wamejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo huo na amewataka mashabiki wa Simba wajitokeze kwa wingi kuisapoti timu yao.
    “Ninawaomba mashabiki wetu waje kwa wingi kutupa sapoti katika kuhakikisha tunaondoka na ushindi kwenye mchezo wa kesho, tumejiandaa vyema kupambana kupata matokeo mazuri na kuondoka na pointi tatu,”amesema.
    Simba SC kwa pamoja na Azam FC, Mtibwa Sugar na Yanga SC zinafungana kwa pointi 12 kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu baada ya kila timu kucheza mechi sita.  
    Mbali na Simba kuwa wenyeji wa Njombe Mji, Azam FC watakuwa wageni wa Mbao FC Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na Mtibwa watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro kesho pia, wakati Yanga SC watakuwa wageni wa Stand United Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga Jumapili.
    Wakati huo huo: Kikosi cha Simba kinatarajiwa kuondoka mapema Jumapili kwenda visiwani Zanzibar kuweka kambi ya kujiandaa na mchezo wao ufuatao wa Ligi Kuu dhidi ya mahasimu, Yanga Oktoba 28 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. 
    Wachezaji wote watakwenda Zanzibar, kasoro majeruhi wa muda mrefu kipa Said Mohammed ‘Nduda’ na mabeki Shomary Kapombe la Salim Mbonde.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SC KUTIMKIA ZENJI BAADA YA MECHI NA NJOMBE KWENDA KUIFANYIA ‘MAARIFA’ YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top