• HABARI MPYA

    Wednesday, October 18, 2017

    SAMATTA ANAVYOPITA KATIKA KIPINDI KIGUMU, MIEZI MIWILI BILA KUFUNGA BAO

    UKAME WA MABAO KWA SAMATTA
    KLABU
    Agosti 13, 2017: Antwerp 3-5 Genk (Alifunga mawili)
    Agosti: 19, 2017: Genk 0-1  Sporting Charleroi (Hakufunga)
    Agosti 26, 2017: Genk 1-0  Mechelen (Hakufunga)
    Septemba 10, 2017: Gent 1-1 Genk (Hakufunga)
    Septemba 16, 2017: Sint-Truiden  2-1 Genk (Hakufunga)
    Septemba 20, 2017: Cercle Brugge 0-1 Genk (Hakufunga)
    Septemba 23, 2017: Genk 1-1 KV Oostende (Hakufunga)
    Septemba 30, 2017: AS Eupen 3-3 Genk (Hakufunga)
    Oktoba 14, 2017: Genk 1-1 Royal Mouscron (Hakufunga)
    TIMU YA TAIFA
    Oktoba 10, 2017;  
    Tanzania 1-1 Lesotho (AFCON) Alifunga kwa penalti dk27
    Setemba 2, 2017;  
    Tanzania 2-0 Botswana (Kirafiki) Hakufunga
    Oktoba 7, 2017:  
    Tanzania 1-1 Malawi  (Kirafiki) Hakufunga
    Mbwana Samatta amefikisha miezi miwili bila kufunga bao hata moja katika klabu yake, KRC Genk nchini Ubelgiji

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amefikisha miezi miwili ya kucheza mechi katika klabu yake, KRC Genk ya Ubelgiji bila kufunga bao.
    Samatta alifunga kwa mara ya mwisho Agosti 13, mwaka huu, KRC Genk ikishinda 5-3 dhidi ya wenyeji, Royal Antwerp FC katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Bosuilstadion, Deurne.
    Siku hiyo, Nahodha huyo wa Taifa Stars alifunga mabao mabao mawili na kuseti mawili na tangu hapo amecheza mechi nane bila kufunga.
    Agosti 13 Samatta alifunga bao la kwanza dakika ya nane na la nne dakika ya 41 na akaseti la pili lililofungwa na mshambuliaji Mbelgiji, Leandro Trossard dakika ya 16 na la tano ambalo beki Mbelgiji, Dino Arslanagic alijifunga dakika ya 59 wakati bao la tatu la Genk lilifungwa na mshambuliaji Mbelgiji, Siebe Schrijvers dakika ya 21.
    Mabao ya Antwerp yalifungwa na kiungo Mbelgiji,  Joeri Dequevy dakika ya 24, mshambuliaji Mghana, William Owusu Acheampong dakika ya 79 na Arslanagic dakika ya 81.
    Oktoba 14, angalau Samatta akafurahi baada ya kutoa pasi iliyoipa bao la kusawazisha KRC Genk ikilazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na Royal Excel Mouscron nyumbani katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk.
    Samatta aliyecheza kwa dakika zote 90, alimsetia Marcus Ingvartsen kuifungia Genk bao la kusawazisha dakika ya 81, baada ya wageni kutangulia kwa bao la Dorin Rotariu aliyeimalizia pasi ya Sebastien Locigno dakika ya 42.
    Hiyo ilikuwa mechi ya 66 kwa Samatta Genk katika mashindano yote tangu Januari mwaka jana alipojiunga na timu hiyo akitokea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
    Mbwana Samatta ameendelea kucheza vizuri na katika kila mechi Genk
    Katika mechi hizo, Samatta ambaye ni mshindi wa tuzo ya Mwanasoka Bora Anayecheza Afrika mwaka jana alipokuwa na Mazembe, 38 ameanza na mechi 24 ametokea benchi.
    Katika mechi hizo, mshambuliaji huyo wa zamani wa African Lyon, zamani Mbagala Market na Simba zote za Dar es Salaam, amefunga jumla ya mabao 21 kwenye mashindano yote.
    Lakini ukifuatilia kupungua kwa makali ya Samatta kunaenda sambamba na kupungua kwa makali ya Genk pia msimu huu, kwa sababu katika mechi zote ambazo Nahodha huyo wa Tanzania hajafunga bao, Genk nayo imeshinda mara mbili tu, tena zote 1-0 dhidi ya Mechelen Agosti 26 nyumbani na Cercle Brugge ugenini Septemba 20, mwaka huu.
    Mechi mbili wamefungwa 1-0 na Sporting Charleroi nyumbani Agosti: 19 na 2-1 na Sint-Truiden ugenini Septemba 16, wakati nne wametoa sare, 1-1 mara tatu dhidi ya Gent Septemba 10 ugenini, KV Oostende, Septemba 23 na Royal Excel Mouscron Oktoba 14 zote nyumbani wakati nyingine wametoka 3-3 na AS Eupen Septemba 30.
    Mwezi uliopita Bin Zubeiry Sports – Online ilifanya mahojiano na Samatta juu ya mwenendo wa kusuasua wa Genk msimu huu na mwenyewe akasema kwamba ushindani umeongezeka katika Ligi Kuu ya Ubelgiji kwa sasa tofauti na ilivyokuwa katika misimu miwili iliyopita wakati anaingia. 
    “Ni hali ya mpira wa miguu tu, kila timu imejiandaa vizuri, kwa hivyo ushindani umeongezeka, umekuwa mkubwa,”alisema Samatta baada ya kuulizwa sababu za makali ya Genk kupungua.
    Sababu nyingi zinatajwa juu ya kupungua kwa makali ya Genk, ikiwemo mabadiliko ya benchi la Ufundi, kufuatia kuondoka kwa kocha Mbelgiji, Peter Maes aliyempokea Samatta mwaka juzi na nafasi yake kuchukuliwa na Mholanzi, Albert Stuivenberg Desemba mwaka jana na pia kuondoka kwa baadhi ya nyota wakiwemo Mnigeria Wilfred Ndidi aliyehamia Leicester City ya England na Mjamaica Leon Bailey, aliyehamia Bayer Leverkusen ya Ujerumani.
    Lakini Samatta haamini sana hayo; “Wachezaji wale waliondoka Januari na baada ya hapo tuliweza kufanya vizuri pia, japo walikuwa msaada mkubwa. Lakini naweza kusema kuna wachezaji walinunuliwa wa kariba inayofanana kwa hivyo nadhani siyo suala la kulifikiria sana,” alisema.
    Mbwana Samatta hajafunga katika mechi mbili zilizopita za Taifa Stars pia
    Yote kwa yote, Samatta anapita katika kipindi kigumu cha kucheza Ligi bila kufunga na wazi hiyo itakuwa inamtia unyonge, kwani inaweza ikamuathiri katika mpango wake wa kusogea kwenye Ligi kubwa zaidi Ulaya, hususan England anakotamani kuhamia wakati wowote.
    Na makali ya Samatta hayajapungua katika klabu yake tu, kwani hata katika timu yake ya taifa nako alifunga mara ya mwisho Oktoba 10, Taifa Stars ikilazimishwa sare ya 1-1 na Lesotho katika mchezo wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon kwa penalti dakika ya 27 kabla ya Thapelo Tale kuwasawazishia wageni dakika ya 34 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Kutoka hapo, Samatta amecheza mechi mbili zaidi Taifa Stars bila kufunga, kwanza ikishinda 2-0 dhidi ya Botswana Septemba 2 na ikitoa sare ya 1-1 na Malawi Oktoba 7, mwaka huu.
    Winga mpya wa Difaa Hassan El Jadida ya Ligi ya Morocco, Simon Happygod Msuva ndiye alikuwa shujaa wa Taifa Stars katika mechi zote hizo mbili, kwanza akifunga mabao yote Septemba 2 katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Botswana dakika ya tano na 63 na akafunga bao la kusawazisha dakika ya 57 katika sare ya 1-1 na Malawi baada ya Nahodha Robert Ng’ambia kuanza kuwafungia wageni dakika ya 35, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Uhuru.
    Samatta anapita katika kipindi kigumu cha kucheza muda mrefu bila kufunga na inaweza ikawa mara ya kwanza hali hii kumtokea katika maisha yake ya soka ya ushindani. Lakini nini kimemsibu? 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA ANAVYOPITA KATIKA KIPINDI KIGUMU, MIEZI MIWILI BILA KUFUNGA BAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top