• HABARI MPYA

    Saturday, October 21, 2017

    OKWI AFUNGA NA KUSETI MAWILI, SIMBA YAUA 4-0 LIGI KUU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI Mganda, Emmanuel Arnold Okwi leo amefunga mabao mawili na kuseti mawili, Simba SC ikiibuka na ushindi wa 4-0 dhidi ya Njombe Mji katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliofanyika Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam.  
    Kwa ushindi huo, Simba inajitanua kileleni mwa Ligi Kuu ikifikisha pointi 15 baada ya kucheza mechi saba.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Hance Mabena, aliyesadiwa na Mohammed Mkono, wote Tanga na Abdallah Rashid wa Pwani, hadi mapumziko, Simba walikuwa mbele kwa bao 1-0. 
    Alikuwa ni kinara wa mabao wa Wekundu hao wa Msimbazi, Okwi aliyewatanguliza Simba dakika ya 27 akifunga kwa kichwa mpira wa juu uliotokana na krosi ya beki wa kulia, Erasto Nyoni aliyeanzishiwa kona na winga Shiza Kichuya.
    Mapema dakika ya kwanza tu, Kichuya alipata pasi nzuri ya kiungo Jonas Mkude, lakini akapiga nje.
    Emmanuel Okwi akipongezwa na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza leo
    Emmanuel Okwi akiwa juu kumalizia krosi ya Erasto Nyoni kuipatian Simba bao la kwanza
    Mfungaji wa mabao mawili ya Simba, Muzamil Yassin akimtoka beki wa Njombe Mji, Jimmy Mwaisondela 
    Mfungaji wa bao la nne la Simba, Laudit Mavugo akimtoka beki wa Njombe Mji, Laban Kambole
    Emmanuel Okwi akimlamba chenga beki wa Njombe Mji, Agathon Mapunda

    Kipa David Kissu na mabeki wake walifanya kazi nzuri ya kuokoa mfululizo baada ya kutokea shambulizi la piga nikupige langoni mwa Njombe Mji dakika ya tano.
    Shuti la Okwi dakika ya 23 likamgonga kifuani Claide Wigenge wa Njombe na kupoteza mwelekeo.
    Kiungo Muzamil Yassin naye alifumua shuti kali dakika ya 40, lakini likaokolewa na kipa Kissu kabla ya mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo naye kuikosesha Simba bao dakika ya 41 baada ya kupiga juu kabisa ya lango kufuatia pasi nzuri ya Kichuya.
    Shambulizi pekee la kusisimua la Njombe lilitokea dakika ya 44 baada ya mshambuliaji Ditram Nchimbi kuwatoka vizuri wachezaji wa Simba na kusogea karibu na boksi, lakini shuti lake halikulenga lango, likaenda nje.
    Kipindi cha pili, Njombe Mji wakatepeta kabisa na Simba kuanza kuutawala mchezo zaidi na kufanikiwa kupata mabao matatu zaidi.
    Kiungo Muzamil Yassin alifunga mabao mawili dakika ya 50 na 52, mara zote akimalizia pasi za Okwi na Mavugo akafunga bao la nne daika ya 58, akimalizia pasi ya Kichuya. 
    Njombe Mji wakabadilisha kipa baada ya mabao hayo, akiingia Rajab Mbululo dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Kissu aliyeumia.
    Kipa wa pili akaenda kulinda vizuri lango la Njombe Mji na kuwazuia Simba kupata mabao zaidi licha ya kuongeza nguvu kwa kuwaingiza Mohammed ‘Mo’ Ibrahim, Nicholaus Gyan na Said Ndemla kuchukua nafasi ya Mavugo, Muzamil na Haruna Niyonzima. 
    Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Yusuph Mlipili, Jonas Mkude, Shizza Kichuya, Muzamil Yassin/Said Ndemla dk74, Laudit Mavugo/Nicholaus Gyan dk61, Emmanuel Okwi na Haruna Niyonzima/Mohammed Ibrahim dk67.
    Njombe Mji FC; David Kissu/Rajab Mbululo dk67, Agathon Mapunda, Innocent Lazaro/ Christopher Kasewa dk59, Ahmed Adiwale, Laban Kambole, Joshua John, Awadh Salum, Jimmy Mwaisondela, Adam Bako/ David Obash dk51, Ditram Nchimbi na Claide Wigenge.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI AFUNGA NA KUSETI MAWILI, SIMBA YAUA 4-0 LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top