• HABARI MPYA

  Thursday, October 19, 2017

  NJOMBE MJI WAWEKA KAMBI MLANDIZI KUJIANDAA NA SIMBA...WANAJIFUA UWANJA WA JESHI

  Na Mwandishi Wetu, PWANI
  TIMU ya Njombe Mji FC imeweka kambi Mlandizi mkoani Pwani tangu juzi kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Simba SC Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Kocha Mkuu wa Njombe Mji, Mrage Kabange ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba wapo Mlandizi tangu juzi wakijiandaa na mchezo huo na wanashukuru maandalizi yao yanaendelea vizuri.
  Kabange amesema kwamba wameweka kambi kwenye moja ya hoteli za wilaya hiyo ambayo hakutaka kuitaja kwa kile alichokieleza kuhofia hujuma na wanafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Mabatini, unaomilikiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambao hutumiwa na timu yao, Ruvu Shooting ya Ligi Kuu pia.
  Kabange amesena wanawafahamu vizuri wapinzani wao, Simba SC ni timu nzuri yenye wachezaji wazuri na wenye uzoefu mkubwa kuliko wa Njombe na ndiyo maana wameamua kujiandaa vizuri zaidi kabla ya mchezo huo ili wapate matokeo mazuri.
  “Tumewaona vizuri Simba wakicheza na Mtibwa Sugar, narudia kusema ni timu nzuri na ndiyo maana tumeupa uzito wa kipekee mchezo huu kwa kuhakikisha tunakuwa na maandalizi mazuri ili tuweze kufanya vizuri,”amesema.    
  Kabange, winga wa zamani wa RTC Kagera na Simba, amesema kikosi cha Njombe FC kitaingia Dar es Salaam kesho tayari kwa mchezo huo wa Jumamosi ambao amekiri utakuwa mgumu.
  Njombe Mji iliyopanda Ligi Kuu msimu huu, itaingia kwenye mchezo wa Jumamosi ikitoka kulazimishwa sare ya 0-0 na jirani zao, Lipuli Uwanja wa Saba Saba Njombe, sawa na wenyeji wao, Simba waliotoa sare ya 1-1 nyumbani na Mtibwa Sugar Uwanja wa Uhuru.
  Njombe Mji ambayo ni timu ya pili ya Njombe kihistoria kucheza Ligi Kuu baada ya Nazareth mwaka 2000, inashika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu ya timu 16, ikiwa na pointi tano, inazidiwa pointi saba na Simba inayoongoza ligi hiyo baada ya mechi sita kuchezwa hadi sasa.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NJOMBE MJI WAWEKA KAMBI MLANDIZI KUJIANDAA NA SIMBA...WANAJIFUA UWANJA WA JESHI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top