• HABARI MPYA

  Monday, October 16, 2017

  NDUDA KUPUMZIKA MIEZI MIWILI BAADA YA UPASUAJI WA GOTI INDIA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KIPA wa pili wa Simba, Said Mohammed 'Nduda' atakuwa nje kwa miezi miwili baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti wiki iliyopita nchini India.
  Daktari wa Simba SC, Yassin Gembe amesema kwamba Nduda anaendelea vizuri baada ya upasuaji huo na sasa atapumzika kwa wiki nane kabla ya kuanza mazoezi mepesi.
  Ikumbukwe Nduda aliyesajiliwa Simba Julai mwaka huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, hajacheza mechi yoyote msimu huu kutokana na maumivu ya goti aliyoyapata Agosti mazoezini.
  Aliumia kambini visiwani Zanzibar wakati Simba inajiandaa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga Agosti 23, mwaka huu Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
  Said Mohammed 'Nduda' atakuwa nje kwa miezi miwili baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti nchini India

  Simba ilivutiwa na Nduda na kumsajili baada ya kudaka vizuri katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu wa Kombe la COSAFA dhidi ya Lesotho Julai 7, mwaka huu mjini Rusternburg, Afrika Kusini Taifa Stars ikishinda kwa penalti baada ya sare ya 0-0. 
  Na Nduda akashinda tuzo ya kipa bora wa mashindano hayo baada ya kazi yake nzuri kwenye mchezo huo mmoja tu, kiasi cha kuwashawishi na Simba kumsajili na kumuunganisha na kipa namba wa Taifa Stars, Aishi Manula.
  Kipa mwingine wa Simba kwa sasa ni Emmanuel Mseja ambaye naye pia ni mpya aliyesajiliwa Julai kutoka Mbao FC ya Mwanza.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NDUDA KUPUMZIKA MIEZI MIWILI BAADA YA UPASUAJI WA GOTI INDIA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top