• HABARI MPYA

    Thursday, October 19, 2017

    MRUNDI AWASILI DAR KUCHUKUA NAFASI YA MAYANJA SIMBA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    MRUNDI Masudi Juma amewasili mchana wa leo nchini kwa ajili ya kuja kusaini mkataba wa kufundisha klabu ya Simba kama kocha Msaidizi.
    Mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Burundi anawasili nchini siku moja tu baada ya aliyekuwa kocha Msaidizi wa Simba, Mganda Jackson Mayanja kung’atuka.
    Baada ya kuwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) mjini Dar es Salaam, Juma alisema kwamba amekuja nchini kuwa kocha Msaidizi wa Simba, chini ya Mcameroon, Joseph Marius Omog.
    “Nimekuja kuwa kocha Msaidizi wa Simba chini ya kocha aliopo kwa sasa. Nataka kusaidia Simba ifanikiwe kutwaa mataji zaidi, najua hiyo ndiyo kiu kubwa,”amesema Juma ambaye mwaka 1995 aliichezea Burundi katika michuano ya Vijana ya Dunia ya FIFA nchini Qatar.
    Masudi Juma amewasili mchana wa leo tayari kusaini mkataba wa kufundisha Simba kama kocha Msaidizi

    Mshambuliaji huyo wa zamani wa Prince Louis ya Burundi, Inter Star za Burundi na Rayon Sport ya Rwanda amesema anafurahi kuja kufundisha Simba timu kubwa Afrika na anaamini atajifunza zaidi, hususan akifanya kazi chini ya kocha mzoefu zaidi, Omog.
    Historia ya ukocha kwa Juma inaanzia mwaka 2013 alipoanza kufundisha timu za vijana za kwao, Burundi kufuatia kustaafu soka mwaka 2010 akiwa na klabu ya Inter Star ya kwao aliyojiunga nayo akitokea Rayon Sport ya Rwanda mwaka 2009. 
    Juma mwenye umri wa miaka 40 ambaye alitua Rayon mwaka 2003 alipojiunga nayo akitokea Prince Louis ya kwao, baada ya kazi nzuri na timu za taifa za vijana za Burundi alirejea Kigali Desemba mwaka 2010 kujiunga na The Blues kama Kocha Msaidizi akichukua nafasi ya Sosthene Habimana, aliyehamia Sunrise FC, chini ya Mbelgiji, Ivan Minneart.
    Juma akateuliwa kuwa Kaimu Kocha Mkuu wa Rayon Februari mwaka jana kufuatia kuondoka kwa Mbelgiji Minneart, hadi mwishoni mwa msimu wa 2015/2016.
    Katika kipindi chake cha kuwa Kocha Mkuu wa Rayon, aliiongoza timu hiyo kutwaa Kombe la Amani kwa mara ya tisa ya rekodi na kwa mara ya kwanza baada ya karibu miaka 11, hivyo kuiwezesha kufuzu Kombe la Shirikisho Afrika ambako walifika kwenye hatua ya mchujo wa kuwania kuingia hatua ya makundi.
    Masudi Juma wakati anawasili mchana wa leo mjini Dar es Salaam tayari kusaini mkataba wa kufundisha Simba 

    Kabla ya kuanza kwa msimu uliopita, Masudi akateuliwa kuwa Kocha Mkuu Agosti mwaka jana kwa mkataba wa miaka mitatu, ambao ulitarajiwa kumalizika mwaka 2020.
    Katika msimu wake wa kwanza, aliiongoza The Blues kutwaa taji la Ligi Kuu ya Azam Rwanda ikiwa na mechi nne mkononi wakimaliza na pointi 73 kutokana na kushinda mechi 22, sare saba na kupoteza mechi moja tu.
    Na wakati wa sherehe za taji la nane la ubingwa wa Ligi ya Rwanda Julai mwaka huu, Juma akwashangaza mashabiki wa Rayon kwa kutangaza kujiuzulu, miezi mitatu tu tangu asimamishwe kwa wiki mbili baada ya timu kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho na Rivers United ya Nigeria akidaiwa kuihujumu timu.
    Wakati wake anacheza Prince Louis, Juma anakumbuka alikutana na Simba katika fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati mwaka 2002 Uwanja wa Amaan, Zanzibar na Wekundu wa Msimbazi wakashinda 1-0 na kubeba taji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MRUNDI AWASILI DAR KUCHUKUA NAFASI YA MAYANJA SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top