• HABARI MPYA

    Monday, October 16, 2017

    MIKOA YATAKIWA KUTHIBITISHA HARAKA USHIRIKI MASHINDANO YA RIADHA YA WANAWAKE

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    VYAMA vya Riadha vya Mikoa yote ya Tanzania Bara na visiwani vimetakiwa kuthibitishwa haraka iwezekanavyo ushiriki wao katika mashindano maalumu ya wanawake yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam, Novemba 25 na 26 mwaka huu.
    Kwa mujibu wa Katibu Msaidizi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Ombeni Zavalla, mashindano hayo yanayofanyika kwa udhamini wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano la Japan (JICA), yatashirikisha wasichana chini ya miaka 20.
    Zavalla, alisema mashindano hayo yanalenga kuibua vipaji na kuhamasisha wanawake kujikita katika mchezo huo kama ilivyokuwa zamani wakati wakifanya vema kitaifa na kimataifa.
    Katibu Msaidizi huyo, alisema vyama vya mikoa yote vimekwishapewa taarifa rasmi isipokuwa mikoa sita pekee, hivyo wanapaswa kuwasiliana na RT kuthibitisha ushiriki wao haraka iwezekanavyo ili mipango ya maandalizi iendelee bila vikwazo.
    “Vyama vya mikoa tayari tumewatumia taarifa rasmi, hivyo wanapaswa kuchagua wachezaji wao wa kuunda timu zao za mikoa na kuanza maandalizi ili kuja kutoa ushindani, lakini kikubwa ni kuwasiliana nasi mara moja kututhibitishia ushiriki wao ili tuendelee na mipango ya maandalizi bila kikwazo,” alisema Zavalla.
    Katibu huyo msaidizi, alifafanua kuwa kila mkoa unapaswa kuwa na wachezaji watano na kiongozi mmoja, ikiwezekana naye awe mwanamke.
    Alisema mikoa itapaswa kugharamia timu zao hadi jijini Dar es Salaam na wakifika gharama zote za malazi na usafiri wa ndani zitagharamiwa na JICA.
    Aliitaja mikoa ambayo imepewa taarifa rasmi ni mikoa mitano ya Zanzibar kupitia Chama cha Riadha Zanzibar (ZAAA).
    Aliitaja mikoa hiyo ni Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kuzini Pemba.
    Kwa bara ni Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mwanza, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Iringa, Mbeya, Njombe, Mtwara, Kigoma, Lindi na Ruvuma.
    Mikoa ambayo vyama vyao ya mikoa haviko hai lakini wamepewa taarifa kupitia Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS), ni Geita, Rukwa, Katavi, Geita na Songwe.
    Katibu huyo msaidizi, alitoa wito kwa wadau mbalimbali mikoani kushirikiana na vyama hivyo ili kuhakikisha wanawawezesha wanawake kushiriki mashindano hayo hasa ukizingatia medali ya kwanza katika mchezo wa riadha hapa nchini ililetwa na Mwanamke, Theresia Dismas mwaka1964.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MIKOA YATAKIWA KUTHIBITISHA HARAKA USHIRIKI MASHINDANO YA RIADHA YA WANAWAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top