• HABARI MPYA

  Sunday, October 15, 2017

  MECHI SITA POINTI MBILI, HII SIYO KAGERA SUGAR TUNAYOIJUA!

  MABINGWA wa zamani wa Kombe la Tusker Challenge, Kagera Sugar jana wamecheza mechi yao ya sita ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara bila ya ushindi.
  Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, Kagera Sugar wamekubali kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa mabingwa watetezi, Yanga SC nyumbani. 
  Kipigo hicho kinaifanya Kagera Sugar ibaki na pointi zake mbili baada ya kucheza mechi sita, tena kati ya hizo tatu wamecheza nyumbani.
  Yanga SC waliondoka wanacheka jana kwa kufikisha pointi 12 baada ya kucheza mechi sita pia na kupanda juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa wastani wa mabao, sasa wakilingana kwa pointi na Azam FC, ambayo jana ililazimishwa sare ya 1-1 na Mwadui mjini Shinyanga.
  Yanga lazima itaondoka kileleni jioni ya leo baada ya mchezo mwingine wa Ligi Kuu baina ya wenyeji, Simba SC na Mtibwa Sugar Uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, kwa sababu hata timu hizo zikitoa sare zitawapita mabingwa watetezi kwa wastani wa mabao.
  Katika mchezo wa jana uliochezeshwa na refa Andrew Shamba wa Pwani, aliyesaidiwa na washika vibendera Joseph Masija na Julius Kasitu pamoja na Jamada Ahmada mezani, hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
  Bao hilo lililofungwa na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 40 aliyemhadaa beki juma Nyosso na kumchambua kipa mkongwe Juma Kaseja, kufuatia pasi nzuri ya mshambuliaji mwenza, Ibrahim Hajib ambaye naye alipasiwa na beki Gardiel Michael.
  Yanga wakaendelea kupeleka mashambulizi langoni mwa Kagera Sugar baada ya bao hilo, lakini Kaseja alisimama imara kuondosha hatari zote hadi filimbi ya kuugawa mchezo ilipopulizwa.
  Na mara baada ya kuanza tu kwa kipindi pili, Yanga wakafanikiwa kupata bao la pili dakika ya 47 lililofungwa na Hajib, baada ya kupewa pasi nzuri na Chirwa.
  Wakati Yanga wakiwa kwenye furaha ya kuongeza bao wakashitukizwa kwa bao la Jaffar Kibaya dakika ya 52 aliyemalizia kwa kichwa krosi ya Venence Ludovic.
  Huo unakuwa mchezo wa pili kwa Kagera Sugar kufungwa nyumbani, baada ya Agosti 26 kufungwa 1-0 na Mbao FC ya Mwanza, kabla ya kuvuna pointi ya kwanza Septemba 10 katika sare ya 1-1 na Ruvu Shooting hapo hapo Kaitaba.
  Mechi nyingine tatu Kagera Sugar wamecheza ugenini, wakifungwa 1-0 na Azam FC Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam na 1-0 na Singida United Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, kabla ya kutoa sare ya 0-0 na Maji Maji mjini Songea. 
  Kichwa kinamuuma bila shaka kocha Mecky Mexime kutokana na matokeo haya, ambayo wazi yanawafanya waajiri wake wamtathmini mara mbili kama anafaa kuendelea kuiongoza timu hiyo.
  Alikuwa ana msimu wa kwanza mzuri uliopita mjini Bukoba akiiwezesha timu hiyo kumaliza katika nafasi ya tatu nyuma ya Yanga na Simba, wakiwapiku Azam FC katika tatu bora maarufu ya Ligi Kuu miaka ya karibuni.
  Kagera Sugar imezoeleka ni timu ya ushindani tangu ilipopanda Ligi Kuu mwaka 2005 na kuwafanya wana Bukoba waishuhudie tena michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu kwa mara ya kwanza tangu walipoipoteza Kagera Stars, zamani RTC Kagera mwaka 2001.
  Mwaka wao wa kwanza Ligi Kuu 2005, walimaliza nafasi ya nne nyuma ya Yanga, Moro United na Simba, mwaka 2006 wakamaliza wa nne pia nyuma ya Yanga, Simba na Mtibwa Sugar na mwaka 2007 hawakufanya vizuri katika Ligi ndogo iliyochezwa kwa makundi.
  Lakini baada ya mfumo mpya wa Ligi Kuu ya kuanzia Agosti, msimu wa 2007-2008, Kagera Sugar ilimaliza nafasi ya tano nyuma ya Yanga, Prisons, Simba na Mtibwa Sugar na msimu wa 2008-2009 ilimaliza nafasi ya sita nyuma ya Simba, Yanga, Mtibwa Sugar, JKT Ruvu na Prisons.
  Msimu wa 2009-2010 ilimaliza nafasi ya saba, 2010-2011 ilimaliza nafasi ya tano, 2011-2012 ilimaliza nafasi ya saba, 2012-2013 ilimaliza nafasi ya nne, 2013-2014 ilimaliza nafasi ya tano, 2014-2015 ilimaliza nafasi ya sita na 2015 – 2016 ilimaliza nafasi ya 12, kabla ya msimu uliopita kurudi juu.
  Ukitazama ushiriki wa Kagera Sugar katika Ligi Kuu utaona ni msimu mmoja tu wa 2015 – 2016 ilifanya vibaya baada ya kumaliza nafasi ya 12 ikinusurika kushuka daraja pamoja na Toto Africans katika msimu ambao Mgambo JKT, African Sports na Coastal Union ziliipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu. 
  Mechi sita za mwanzo katika msimu wa 2017 -2018 Kagera Sugar siyo haijashinda, bali imeambulia pointi mbili katika Ligi Kuu ambayo inaonekana kuwa ya ushindani zaidi ukilinganisha na msimu uliotangulia. Hii siyo Kagera Sugar tunayoijua.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MECHI SITA POINTI MBILI, HII SIYO KAGERA SUGAR TUNAYOIJUA! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top