• HABARI MPYA

  Wednesday, October 18, 2017

  MAYANJA AACHANA NA SIMBA, MBADALA WAKE KUTANGAZWA KESHO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MGANDA Jackson Mayanja ameachana na klabu ya Simba baada ya kufanya nayo kazi kwa karibu miaka miwili.
  Mayanja ameaga rasmi leo na kuondoka Simba, akisema sababu binafasi ndizo zinamuondoa kwenye timu, huku taarifa nyingine zikisema ni uongozi umeamua kuachana naye.
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Hajji Sunday Manara amethibitisha kujiuzulu kwa kiungo huyo wa zamani wa kimataifa wa Uganda alipozungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo mjini Dar es Salaam.
  Manara amesema kufuatia kuondoka kwa Mganda huyo, klabu itamtangaza kocha mpya Msaidizi kesho ambaye ataanza kazi mara moja kuelekea mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Njombe Mji FC Jumamosi Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Mayanja aliingia Simba Januari mwaka jana kama Kocha Msaidizi akitokea Coastal Union ya Tanga, kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa Kocha Msaidizi, Suleiman Matola Novemba mwaka 2015.
  Jackson Mayanja (kulia) ameachana na klabu ya Simba baada ya kufanya nayo kazi kwa karibu miaka miwili

  Mechi chache kabla ya kumalizika kwa msimu wa 2015-2016, aliyekuwa Kocha Mkuu, Muingereza Dylan Kerr akaondolewa na Mayanja akaanza kukaimu Ukocha Mkuu hadi mwisho wa msimu.
  Aliiongoza timu katika mechi 22, ikishinda 15, sare mbili na kufungwa tano kama Kaimu Kocha Mkuu, kabla ya kuja kwa Mcameroon, Joseph Marius Omog kuziba nafasi ya Kerr na Mganda huyo kurejeshwa kuwa Msaidizi tena.  
  Na akiwa msaidizi wa Omog Simba imecheza jumla ya mechi 67, ikishinda mechi 46, kufungwa nane na sare 10.
  Haijulikani Mayanja ambaye klabu yake ya kwanza kufundisha nchini ni Kagera Sugar ya Bukoba atakwenda wapi baada ya kuondoka Simba.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MAYANJA AACHANA NA SIMBA, MBADALA WAKE KUTANGAZWA KESHO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top