• HABARI MPYA

    Friday, October 20, 2017

    KABLA YA KUIVAA MBAO, AZAM WAWATEMBELEA YATIMA MWANZA

    Na Mwandishi Wetu, MWANZA
    IKIWA imesalia siku moja kabla ya kikosi cha Azam FC hakijakabiliana na Mbao, Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati muda mchache uliopita asubuhi hii wametembelea kituo cha watoto yatima cha Sekondari ya Ilemela Islamic Seminary, kilichopo Ilemela mkoani Mwanza.
    Mabingwa hao wanatarajia kumeanyana na Mbao kesho Jumamosi katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, mjini hapa.
    Beki wa Azam FC, Aggrey Morris (kulia) akiwahutubia wanafunzi wa kituo cha watoto yatima wa sekondari ya Kiislamu ya iliyopo Ilemela mkoani Mwanza baada ya kuwatembelea leo. 
    Hapa Nahodha Himid Mao anakabidhi mpira kwa mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo kama moja ya zawadi walizowapelekea 
    Wachezaji wa Azam FC wakiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi wa shule hiyo

    Huo ni mwendelezo wa klabu hiyo katika kujenga mahusiano mazuri na jamii kwa kujali watu wenye mahitaji mbalimbali, ambapo mwaka jana mwishoni ilitoa msaada kwa baadhi ya wakazi wa mkoa wa Kagera walioathirika na tetemeko la ardhi ilifanya hivyo siku kadhaa kabla ya kukabiliana na Kagera Sugar na kufanikiwa kushinda kwa mabao 3-2.
    Zoezi hilo limehudhuriwa na msafara wote wa Azam FC uliowasili mkoani hapa Mwanza, ambapo wamepokelewa kwa heshima kubwa na viongozi wa seminari hiyo wakiongozwa na Meneja na Makamu Mwenyekiti, Sherally Hussein Sherally.
    Azam FC haijaiacha mikono mitupu Seminari hiyo inayotoa elimu ya awali, msingi na sekondari kwa ngazi zote mbili, kwani imetoa msaada wa katoni 10 za Maji safi ya Uhai Drinking Water, Katoni mbili za Juice za boksi za Azam na mbili nyingine za kopo pamoja na pakiti mbili za pipi.
    Uongozi wa seminari umeipongeza na kuishukuru timu hiyo na Kampuni kwa ujumla ya Azam kwa moyo wa huruma waliouonyesha na kuamua na kuitakia mafanikio mema kwenye mechi wanazocheza.
    Wakati huo huo: Kipa namba moja, Mghana Razak Abalora, kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na mshambuliaji nyota Mbaraka Yusuph wameteuliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Azam FC mwezi Septemba.
    Tuzo hiyo iliyoanza kutolewa Agosti mwaka huu ikidhaminiwa na Mdhamini Mkuu wa Azam FC, Benki bora kabisa nchini ya NMB, ilishuhudiwa beki kisiki Yakubu Mohammed akiitwaa kwa mara ya kwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KABLA YA KUIVAA MBAO, AZAM WAWATEMBELEA YATIMA MWANZA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top