• HABARI MPYA

    Sunday, September 03, 2017

    TUNAHITAJI LIGI DARAJA LA KWANZA BORA NA SI UTITIRI WA TIMU LIGI KUU

    KUANZIA msimu ujao wa 2018/2019, Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara itakuwa na timu 20 badala ya 16 za sasa.
    Maamuzi hayo yalifikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Agosti 22, mwaka huu, ambacho kilifanyia marekebisho Kanuni za Ligi Daraja la Kwanza inayotarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu.
    Baada ya marekebisho hayo, sasa timu mbili tu zitashuka daraja msimu huu kutoka Ligi Kuu na 14 zitakazobaki zitaongezewa timu nne zitakazopanda kutoka Daraja la Kwanza ili kufikisha idadi ya timu 20 kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu.
    Kwa mujibu wa utaratibu wa Ligi Daraja la Kwanza, ina maana kwamba msimu huu timu mbili zitapanda kutoka katika kila kundi katika ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuanza Septemba 16, mwaka huu.
    Sababu zinazotajwa na TFF kuongeza timu Ligi Kuu ni imani kwamba idadi ya mechi zitaongezeka na wachezaji watakuwa na wigo mpana zaidi wa kujipambanua. Hizi ni imani tu na matarajio ya viongozi wa TFF, ambazo ukienda kwenye uhalisia unaweza kuanza kuyatilia shaka maamuzi hayo.
    Inaonekana nia ya kuongeza timu katika Ligi Kuu ni nzuri tu kutaka kuikuza zaidi Ligi na kuwajenga wachezaji pia, lakini kuna wasiwasi wazo hilo halikufanyiwa kazi kiasi cha kutosha.
    Soka ya Tanzania imepoteza uhondo wake kutokana na kupungua kwa wachezaji bora na vipaji vya aina ya wachezaji wa kuanzia miaka ya 1970 hadi 2000. Tunakumbushia zama ambazo wachezaji wa Tanzania, kipa Omar Mahadhi na mshambuliaji Maulid Dilunga (wote marehemu sasa) wakiwa wanacheza Ligi ya nyumbani walichaguliwa kombaini ya Afrika, mwaka 1973 baada ya Michezo ya Afrika Jijini Lagos, Nigeria.
    Sawa, mwaka jana mchezaji wa Tanzania, Mbwana Samatta alishinda tuzo ya Mwanasoka Bora Afrika Anayecheza barani, lakini alikuwa anatokea Ligi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) alipokuwa na klabu ya TP Mazembe iliyomsaidia kuonekana Ulaya na sasa anacheza KRC Genk ya Ubelgiji.
    Ukweli ni kwamba tuna tatizo sehemu, lakini inasikitisha sana wataalamu wote waliosheheni pale TFF na Bodi ya Ligi wameshindwa kuling’amua na badala yake wanataka kutuaminisha dawa ni kuongeza idadi ya timu Ligi Kuu.
    Makamu wa Rais wa sasa wa TFF, Michael Richard Wambura atakuwa anakumbuka vizuri akiwa Katibu Mkuu chini ya Mwenyekiti, Muhiddin Ndolanga waliongeza idadi ya timu Ligi Kuu hadi 20, lakini matokeo yake msimu uliofuata wakarudi kwenye ligi ya timu 16.
    Ilikuwa ni mzigo tu, timu nyingi zilikuwa hazijiwezi kwa hali wala mali zikaleta usumbufu mkubwa hadi wa kutofika vituoni, achilia mbali kufungwa idadi kubwa ya mabao.
    Sawa, unaweza kusema wakati huo wadhamini walikuwa wachache Ligi Kuu na sasa kuna Vodacom na Azam TV na hata klabu zenyewe zinaweza kuja na ngekewa ya Singida United ya kupata wafadhili wengi, lakini bado huwezi kuukwepa ukweli wa tatizo liliopo na la msingi katika soka yetu.
    Tatizo ni kutokuwa na Ligi imara za madaraja ya chini – likiwemo la kwanza ambalo ndilo msingi mkuu wa kuwa na timu bora za Ligi Kuu. Tumekuwa na Ligi Daraja la Kwanza ya kisanii tu, ya makundi inayotakiwa kuisha haraka ili timu za kupanda zipatikane na kwa sasa imekuwa rahisi mno kupanda Ligi Kuu ndiyo maana timu kama Toto, African Lyon, Ruvu Shooting hivi karibuni zimepanda na kushuka mapema tu.
    Miaka ya 1990 Ligi Daraja la Tatu Mkoa, ilikuwa ni Ligi yenye msisimko wa hali ya juu – na baada ya hapo ukiingia kwenye Ligi Daraja la Tatu Kanda huko ndiko moto zaidi ulikuwa unawaka kabla ya kupata timu za kwenda Daraja la Pili, ambako kulikuwa kugumu zaidi. Nakumbuka miaka hiyo kuna timu zilikuwa alama ya Ligi Daraja la Pili, kwa sababu zilikuwa hazishuki wala hazipandi, lakini ni za upinzani.
    Na ukienda Daraja la Kwanza timu zilizokuwa zinapanda Ligi Kuu ziliingia na wachezaji wake wale wale iliyopanda nao na kwenda kuwa tishio, tofauti na sasa timu ikipanda Ligi Kuu inabomoa karibu kikosi kizima na kusajili wachezaji wapya.
    Inakuwaje timu inapanda Ligi Kuu halafu inafukuza wachezaji walioisaidia kupanda – wakati mwaka juzi tu England Leicester City ilipanda na wachezaji wake ikaenda kuchukua hadi ubingwa wa Ligi Kuu – mambo kama ambayo hapa nyumbani yalifanywa na Tukuyu Stars ya Mbeya mwaka 1986 ilipanda Ligi Kuu na moja kwa moja kwenda kuchukua ubingwa na wachezaji wake wakawa nyota wa taifa. 
    Lakini kinachoumiza zaidi, Ligi Daraja la Kwanza imedharauliwa mno na sasa imekuwa ni hatua tu ya kupata timu za kwenda Ligi Kuu tu, wakati yenyewe pia ni bidhaa na eneo la kututengenezea bidhaa bora zaidi za kupeleka Ligi Kuu.
    Siku hizi tuna ligi za makundi, Kundi A zinapanda mbili, Kundi B zinapanda mbili – wakati tunapaswa kuwa na Ligi ya kutoa bingwa wa Daraja la Kwanza na timu zinazofuatia za kupanda. Tumeshindwa kuifanya Ligi Daraja la Kwanza iwe kitu chenye thamani pamoja na uzito wake, tutarajie nini sasa huko kwenye Ligi za chini zaidi kuanzia Daraja la Pili kuendelea?    
    Nakumbuka mwaka 1999 mchezaji wa Reli Kigoma iliyokuwa Daraja la Pili, Said Maulid ‘SMG’ alichaguliwa moja kwa moja timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars na ikawa njia pia ya kusajiliwa kwake Simba kabla ya kuwa nyota miaka ya 2000 hadi kucheza Angola.     
    Miaka hiyo ilikuwa jambo la kawaida mchezaji kuchukuliwa timu ya taifa kutoka timu ya Daraja la Kwanza, kwa sababu walikuwa wana uwezo mkubwa kweli kutokana na mfumo wa wakati huo.
    Nataka niwaambie viongozi wa TFF, kukimbilia kuongeza timu Ligi Kuu ni kujidanganya tu, kwani tatizo letu ni kuitelekeza Ligi Daraja la Kwanza na kuifanya kama kijiwe cha kutupatia timu za kupanda Ligi Kuu, badala ya kuifanya iwe na hadhi na thamani kubwa sawa na umuhimu wake.
    Tunahitaji Ligi Daraja la Kwanza itakayoendeshwa kama ilivyo Ligi Kuu yetu sasa, tena huko ndiko tunaweza kuwa na timu 20 au zaidi kila timu icheze na timu nyingine zote nyumbani na ugenini na mwisho wa msimu tupate timu madhubuti za kupanda Ligi Kuu. Baada ya hapo, tuboreshe na Ligi za chini yake hadi kuhakikisha mfumo wa soka yetu unakuwa imara tena. Kwa sasa kuongeza timu Ligi Kuu ni kujidanganya tu, tuboreshe Daraja la Kwanza.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TUNAHITAJI LIGI DARAJA LA KWANZA BORA NA SI UTITIRI WA TIMU LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top