• HABARI MPYA

    Tuesday, September 12, 2017

    TFF YAPANUA ‘KIWANDA CHA MAKOCHA’ NCHINI

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limeongeza juhudi za kufundisha makocha wa mpira wa miguu hapa nchini ili idadi ya walimu wa mpira wa miguu wanaopaswa kushiriki kwenye programu za maendeleo ya vijana za mikoa.
    Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas amesema leo mjini Dar es Salaam kwamba hiyo ni katika kukidhi malengo ya TFF katika kusimamia maendeleo ya soka la vijana hapa nchini. 
    Lucas ameseam kwamba kwa sasa, TFF kwa kushirikiana na mikoa ya Songwe, Lindi na Kigoma, zinaendeshwa kozi ngazi ya awali (Preliminary) na ngazi ya kati (Intermidiate).
    “Katika mkoa wa Songwe kozi ya ukocha zinazoendeshwa ni kozi ya awali Wilaya ya Songwe inayoendeshwa na Mkufunzi John Simkoko na kozi ya awali, wilaya ya Tunduma inaendeshwa na Mkufunzi George Mkisi,”.
    Mmoja wa makocha vijana nchini waliozalishwa hivi karibuni, Zubeiry Katwila wa Mtibwa Sugar

    “Mkoani Lindi kozi ya awali ilianza Septemba 11, 2017 katika Wilaya ya Kilwa ikiendeshwa na Mkufunzi Michael Bundala na mkoani Kigoma kuna kozi mbili zinaendelea,” amesema.
    Ofiosa huyo wa TFF amesema kwamba kozi moja ni ya ngazi ya awali ambayo inaendeshwa na Mkufunzi George Komba na kozi Ngazi ya Kati inaendeshwa na Mkufunzi Rogasian Kaijage.
    Wakati huo huo: TFF imeishukuru Serikali ya Mkoa wa Dar es Salaam; Mkuu wa Wilaya Temeke jijini pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama kwa namna walivyoshirikiana na Shirikisho katika kusimamia mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara uliokutanisha timu za Azam FC na Simba.
    Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam Jumamosi iliyopita Septemba 9, mwaka huu, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
    Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred ameshukuru vyombo vya ulinzi na usalama kusimamia utaratibu wa weledi katika kudhibiti kila aina ya vurugu kabla, wakati na baada ya mchezo huo.
    “Watu wote walifika uwanjani kwa utulivu, walikaa vema uwanjani, baadaye waliondoka bila ya vurugu yoyote. Hakuna tukio lililolipotiwa kwangu kwamba kuna vurugu eti kwa sababu ya mechi… hakuna,” amesema Kidao.
    Ameongeza: “Mchezo ulikuwa mzuri, nadhani kila aliyekuja uwanjani anaweza kuwa shahidi. Hii inatupa nguvu kwamba siku nyingine tunaweza kuandaa mchezo mwingine mkubwa katika uwanja ule.”
    Amesema kwamba nguvu ya kuandaa mchezo mwingine mkubwa katika Uwanja wa Azam ni nguvu ya ushirikiano aliyoipata kutoka Serikali ya Mkoa chini ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TFF YAPANUA ‘KIWANDA CHA MAKOCHA’ NCHINI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top