• HABARI MPYA

    Thursday, September 14, 2017

    TANZANITE YAENDA KUMENYANA NA NIGERIA KUFUZU KOMBE LA DUNIA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania ya wanawake chini ya umri wa miaka 20 ‘The Tanzanite’ imeondoka usiku wa kuamkia leo Alhamisi kwenda Nigeria kwa Ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia.
    Timu hiyo inakwenda Nigeria kucheza na wenyeji katika mchezo kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia. Fainali hizo za vijana kwa wasichana, zitafanyika Ufaransa, mwakani.
    Mchezo utafanyika Septemba 16, mwaka huu katika Uwanja wa Samuel Ogbemudia uliko Jiji la Benin kabla ya kurudiana na Tanzania wiki mbili zijazo katika uwanja na tarehe ambayo TFF itaitangaza baadaye.
    Timu imeondoka na wachezaji 20 na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sebastian Nkoma amesema wana matumaini ya kufanya vema kwenye mchezo huo ilihali Nahodha wa timu hiyo, Wema Richard akiaminisha Watanzania kurudi na ushindi akisema: “Hapa ni kazi kazi.”
    Timu hiyo iliagwa kwa kupewa Bendera ya Taifa jana Jumatano Septemba 13, mwaka huu na Mkurugenzi wa Michezo, Yussuph Singo na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred ambao kila mmoja aliwatakia kila la kheri vijana hao.
    Singo, alisema: “Namshukuru Mungu kwanza kiafya mko vizuri. Tunawaombea muendelee kuwa na afya njema; shukrani kwa TFF kuwatunza vema na kuwapa posho. silaha yenu kubwa ni nidhamu kwa sababu bila nidhamu hamuwezi kufanikiwa.
     “Kwa niaba ya Serikali, nawatakia safari njema na mafanikio katika mchezo. Mkiwafunga Nigeria, nitamshawishi Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuja kuwapokea hata kama mtarejea usiku wa manane,” amesema.
    Katika kikosi hicho, kuna makipa watatu ambao ni Agatha Joel, Zainab Abdallah na Gelwa Mgomba wakati Walinzi ni Eva Jackson, Aquila Gasper, Asphat Kasindo, Ester Mayala, Silivia Mwacha,  Stella Wilbert, Wema Richard,  Hadija Ali, Rukia Anafi na Christine Daudi.
    Viungo ni Herieth Shija, Julieth Singano na Shamimu Hamis na Washambuliaji ni Veronica Mapunda, Opa Clement, Zainabu Mohamed na Philomena Daniel. Kila la kheri The Tanzanite.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TANZANITE YAENDA KUMENYANA NA NIGERIA KUFUZU KOMBE LA DUNIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top