• HABARI MPYA

    Monday, September 04, 2017

    SIMBA YAUNDA KAMATI YA KUTAFUTA WANUNUZI WA HISA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    SIMBA SC leo imetaja Kamati Maalum ya Kusimamia mchakato wa zabuni ya kumpata mwekezaji katika mfumo mpya wa uendeshwaji wa klabu.
    Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu, Hajji Sunday Manara amesema kwamba Kamati hiyo itakuwa chini ya Mwenyekiti, Jaji Mstaafu, Thomas Mihayo.
    Manara amesema Mihayo atakuwa na Wajumbe wanne katika Kamati hiyo, ambao ni Mbunge wa jimbo la Ilala (CCM), Mussa Azzan ‘Zungu’, Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu, Abdulrazaq Badru, Wakili maarufu katika masuala ya michezo Dk. Damas Ndumbaro na mtaalamu aliyebobea katika masuala ya Ununuzi, Yussfu Maggid.

    Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Salim Abdallah 'Try Again' katika mkutano wa Agosti 20, mwaka huu

    Manara amewataka wanachama wa klabu hiyo kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha mchakato wa mageuzi ya kiuendeshaji ndani ya klabu.   
    Agosti 20, mwaka hu wanachama 1,216 wa klabu ya Simba waliridhia mfumo wa klabu yao kuuza Hisa baada ya Mkutano uliofanyika Ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Nyerere (MNICC), Dar es Salaam.
    Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Waziri wa Afya Jinsia na Watoto, Dk Hamisi Kigwangala, Kaimu Mwenyekiti wa klabu, Salim Abdallah 'Try Again' alisema kwamba asilimia 50 ya hisa zitauzwa kwa mwekezaji yeyote au wowote watakaoungana wasiozidi watatu, kwa sharti moja tu la kuwa wanachama wa klabu hiyo. 
    Abdallah alisema mwekezaji huyo au hao, wanatakiwa kuweka dau lisilopungua Sh. Bilioni 20 ili kupatiwa asilimia 50 ya hisa za klabu, wakati kwa kuanzia wanachama wote wa Simba wamepewa asilimia 10 ya hisa.
    Alisema asilimia nyingine 40 zitawekwa kama mtaji wa klabu na zitauzwa kwa wanachama baadaye, lakini wale wawekezaji walionunua asilimia 50 awali, hawataruhusiwa kununua hata hisa moja kwenye asilimia 40 za mtaji.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA YAUNDA KAMATI YA KUTAFUTA WANUNUZI WA HISA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top