• HABARI MPYA

  Friday, September 01, 2017

  SIMBA KUCHEZA NA WANAJESHI WA ZANZIBAR JUMAPILI UHURU

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  MCHEZO wa kirafiki kati ya Simba SC na Hard Rock ya kisiwani Pemba utafanyika Jumapili ya Septemba 3, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
  Awali mchezo huo ilikuwa ufanyike jioni ya leo, lakini uongozi wa Simba ukaamua kuupeleka Jumapili ili kupisha maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa kimataifa kati ya wenyeji, Tanzania na Botswana.
  Taifa Stars watakuwa wenyeji wa The Zebras (Pundamilia) katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Jumamosi jioni Uwanja wa Uhuru.
  Na katika matayarisho ya mchezo huo, Botswana leo jioni wanafanya mazoezi kwenye Uwanja huo, hivyo haitawezekana mchezo wa kirafiki kati ya Simba na Hard Rock, timu ya Jeshi la Zanzibar kufanyika hapo leo.
  Mashabiki wa Simba wanakaribishwa tena Jumapili Uwanja wa Uhuru kwenda kumuona Haruna Nayonzima na 'shoo' zake za kusisimua 
  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba, Hajji Sunday Manara ‘De La Boss’amesema kwamba wanawaomba radhi wapenzi na wanachama wao kwa usumbufu wowote na wanawasihi kujitokeza kwa wingi Jumapili Uwanja wa Uhuru kuisapoti timu yao.
  “Nitumie fursa hii adhimu kutoa salaam za mkono wa Eid (El Haj), kutoka kwa uongozi mzima wa klabu, kuanzia Kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’, Kamati ya Utendaji, Sekretarieti chini ya Katibu Mkuu, Dk Arnold Kashembe, wanachama, mashabiki, wachezaji na benchi zima la ufundi kuwatakiwa Watanzania wote heri na fanaka kwenye sikukuu hii inayosheherekewa kote duniani, ikiambatana na ibada tukufu ya Hijja, ambayo ni nguzo ya tano ya Uislaam,”amesema Manara. 
  Pamoja na hayo, Manara ameitakia mchezo mwema Taifa Stars Jumamosi, huku akiipongeza Uganda kwa ushindi wa 1-0 jana kwenye mchezo wa Kundi E kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Misri, bao pekee la mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi Uwanja wa Mandela, Namboole, Kampala.
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA KUCHEZA NA WANAJESHI WA ZANZIBAR JUMAPILI UHURU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top