• HABARI MPYA

    Sunday, September 03, 2017

    SAMATTA AMWAGIA SIFA YONDAN, ASEMA MKONGWE AMERUDI NA UBORA WAKE

    Na Prince Akbar, DAR ES SALAAM
    NAHODHA wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amemsifu beki mkongwe, Kevin Patrick Yondan kwa kuonyesha kiwango kizuri katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa jana Taifa Stars ikishinda 2-0 dhidi ya Botswana Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Yondan alijiondoa kwenye kikosi cha Taifa Stars baada ya kipigo cha mabao 7-0 kutoka kwa wenyeji, Algeria Jumanne ya Novemba 17, mwaka 2015 kwenye mchezo wa  kufuzu Kombe la Dunia kabla ya kurejea jana na kuingoza Taifa Stars kushinda 2-0.
    Na baada ya mchezo huo, Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji, akasema kwamba amefurahishwa na kiwango cha beki wa Yanga ya nyumbani, Tanzania, Yondan ambaye amerejea kikosini baada ya takriban miaka miwili. 
    Mbwana Samatta (katikati) amemsifu Kevin Yondan (kushoto) kwa mchezo mzuri jana akirejea kikosini Taifa Stars baada ya miaka miwili 
    Samatta pia akampongeza mfungaji wa mabao yote mawili kwenye ushindi wa jana, winga mpya wa Difaa Hassan El Jadida ya Morocco, Simon Msuva huku akisema kipigo ni halali yao Botswana jana.
    “Botswana walijitahidi ila ilikuwa lazima wafungwe maana hawana kikosi bora zaidi yetu. Tungeshangaa kama sisi tusingeshinda, maana hatuna sababu kwa sasa,”alisema.
    Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema amefurahishwa na wachezaji ambao amewaita kwa mara ya kwanza katika kikosi hicho na akiahidi kuzidi kuwapa nafasi wengine ambao hajawahi kuwaita.
    Ushindi huo wa Taifa Stars ni sita kwa Mayanga toka akabidhiwe mikoba ya kukinoa kikosi hicho kutokea kwa Charles Boniface Mkwassa ambaye sasa ni Katibu Mkuu wa Yanga.
    Lakini, Mayanga ameiongoza Taifa Stars kucheza mechi 12, ambazo sita akishinda, tano akitoka sare na kufungwa mechi moja.
    Mayanga alisema kuwa amefurahishwa na uwezo wa wachezaji ambao wameonyesha hata kama ilikuwa mechi yao ya kwanza.
    “Wengi mlikuwa mnapiga kelele kuhusu kuchukua wachezaji ambao wanacheza nje ya nchi. Hivyo tumeanza kuyafanyia kazi na ndio maana tumeanza kuwapa nafasi kama Hamisi Abdallah. Tumempa muda mwingi ili watu wamuone na tutazidi kuwatumia vijana wapya zaidi na tuje kuwa na timu ya taifa imara,”alisema.
    Kocha Mkuu wa Botswana 'The Zebras', David Bright yeye alimsifu kipa Stars, Aishi Manula ambaye anaona amekuwa kizingiti kikubwa cha wao kukosa matokeo chanya.
    “Kwangu mimi yule kipa ni mzuri, naweza kusema ni kipa wa maajabu. Katika mchezo wa leo (jana) naweza kusema ndio mchezaji bora wa mechi kwani alicheza vizuri kwenye eneo lake,”alisema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SAMATTA AMWAGIA SIFA YONDAN, ASEMA MKONGWE AMERUDI NA UBORA WAKE Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top