• HABARI MPYA

    Sunday, September 17, 2017

    OKWI NI MCHEZAJI BORA WA WIKI, AU MWEZI LIGI KUU?

    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ilianza Agosti 26, mwaka huu kwa mechi saba kuchezwa kwenye viwanja tofauti nchini.
    Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara wenyeji Ndanda FC walifungwa 1-0 na Azam FC, Uwanja wa Sokoine, Mbeya City walishinda 1-0 dhidi ya Maji Maji, Uwanja wa Saba Saba wenyeji Njombe Mji wakafungwa 2-0 na Tanzania Prisons na Uwanja wa Kaitabam, Bukoba Kagera Sugar wakafungwa 1-0 na Mbao FC.
    Mechi nyingine, Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Simba wakashinda 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting, Uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar wakashinda 1-0 dhidi ya Stand United, Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga wenyeji, Mwadui wakashinda 2-1 dhidi ya Singida United.
    Mchezo wa mwisho wa Ligi Kuu mzunguko wa kwanza kabisa ulihitimishwa Agosti 27, mabingwa watetezi, Yanga SC wakilazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli ya Iringa iliyopanda msimu huu.
    Baada ya hapo, Ligi Kuu ikaenda mapumzikoni kupisha kalenda ya mechi za kimataifa zikiwemo za kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Urusi, kabla ya kurejea Septemba 9, yaani wiki iliyopita.
    Lakini kabla ya kuingia kwenye mechi za pili za Ligi Kuu, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likamtangaza mshambuliaji Mganda wa Simba, Emmanuel Arnold Okwi kuwa mchezaji bora wa Mwezi Agosti wa Ligi Kuu, eti akiwashinda kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohammed Issa na beki wa Mbao FC, Boniface Maganga.
    Katika mechi za kwanza za Ligi Kuu, Okwi aling’ara zaidi baada ya kufunga mabao manne katika ushindi wa 7-0 akiweka rekodi ya mchezaji wa kwanza kufunga hat trick msimu huu, wakati Mohammed Issa aliisaidia Mtibwa kushinda 1-0 nyumbani dhidi ya Stand United na Maganga aliiwezesha Mbao kushinda ugenini 1-0 dhidi ya Kagera Sugar. 
    Hakuna ubishi kwamba Okwi aling’ara zaidi baada ya mechi za kwanza kwa sababu alifunga hat trick na inajieleza wazi na huo ulikuwa mtaji mzuri kwake kuelekea kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi kama Ligi Kuu ingechezwa kwa mwezi.
    England Mchezaji Bora wa baada ya mechi chache zaidi ni mbili, ambazo huchezwa ndani ya wiki mbili, lakini hii ya mechi moja ya Uchezaji Bora wa Okwi inataka kuwa rekodi ya dunia hapa kwetu.
    Hakuna wa kulaumiwa hapa zaidi ya Bodi ya Ligi iliyopanga Ratiba ya kuifanya Ligi Kuu ichezwe kwa raundi moja tu mwezi Agosti, wakati kulikuwa kuna uwezakano wa ligi hiyo kuanza kabla ya hapo ili kutoa fursa ya mechi zaidi katika mwezi wake wa kwanza ili kutengeneza mazingira ya kupata Mchezaji Bora wa Mwezi kwa maana ya Mwezi na si huyu wa Agosti aliyepatikana baada ya wiki.   
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: OKWI NI MCHEZAJI BORA WA WIKI, AU MWEZI LIGI KUU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top