• HABARI MPYA

    Sunday, September 10, 2017

    MSUVA AANZA KWA SARE LIGI KUU MOROCCO

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva jana amecheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola, Difaa Hassan El –Jadida ikilazimishwa sare ya 0-0 nyumbani na Chabab Atlas Khenifra Uwanja wa Ben Ahmed El Abdi mjini El Jadida, Mazghan. 
    Huo ni mchezo wa pili wa mashindano kwa Msuva tangu ajiunge na timu hiyo baada ya wiki mbili zilizopita kuisaidia Difaa Hassan El-Jadida kufuzu kwenye Raundi ya Pili ya michuano ya Kombe la Ligi Morocco, maarufu kama Throne Cup kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya CR Khemis Zemamra Uwanja wa Grand Prix mjini Marrakech.
    Simon Msuva (wa pili kulia) katika kikosi cha kwanza cha Difaa Hassan Dl Jadida jana 
    Hapa tayari wamevua jezi kwa ajili ya kuingia uwanjani kwa ajili ya mchezo mgumu ulioisha kwa sare ya 0-0

    Siku hiyo Msuva aliyejiunga na Difaa Hassan El-Jadida Julai akitokea kwa mabingwa wa Tanzania, Yanga SC alifunga bao la tatu dakika ya 62, baada ya beki Marwan Aghudy kufunga bao la kwanza dakika ya 28 na mshambuliaji Bilal Almkra kufunga la pili dakika ya 34.
    Tayari Msuva amefunga mabao saba tangu amejiunga na timu hiyo, mengine sita akifunga kwenye mechi za kirafiki, zikiwemo za ziara ya Hispania.  
    Msuva alisaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na DHJ Julai 28, mwaka huu baada ya kucheza  Yanga ya nyumbani, Tanzania tangu mwaka 2012 akitokea Moro United iliyokuwa tayari imehamishia maskani yake Dar es Salaam kutoka Morogoro.
    Awali ya hapo, Msuva alipitia akademi ya Azam akitokea kituo cha kukuza vipaji vya wanasoka chipukizi, Wakati Ujao baada ya kuibuliwa na iliyokuwa taasisi ya Pangollin ya kocha Charles Boniface Mkwasa, ambaye sasa ni Katibu wa Yanga, klabu aliyoichezea na kuifundisha awali.. 
    Na baada ya kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mfungaji bora mara mbili – Msuva amehamia Morocco kusaka changamoto mpya na mafanikio zaidi kisoka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MSUVA AANZA KWA SARE LIGI KUU MOROCCO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top