• HABARI MPYA

    Tuesday, September 12, 2017

    JKT OLJORO, RUVU ZAPANIA KUPAMBANA DARAJA LA KWANZA ZIRUDI LIGI KUU

    Na Clement Shari, ARUSHA
    TIMU ya soka ya JKT Oljoro ya Arusha imesema ipo tayari kuanza kucheza mechi za Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara mara baada ya kufanikiwa kurejea katika ligi hiyo kufuatia kushushwa daraja misimu miwili iliyopita.
    Kocha mkuu wa JKT Oljoro, Emmanuel Massawe ameiambia Bin Zubeiry Sports – Online leo kwamba kikosi chake kipo kamili na kwa sasa anamalizia mambo madogo madogo ikiwemo mikakati ya mechi zao, lakini kwa ujumla kila kitu kipo sawa.
    Massawe amesema wachezaji wote wapo vizuri isipokuwa wachezaji wawili waliokuwa majeruhi ambao wamekwisharejea kikosini na kuanza mazoezi mepesi.
    Kocha wa JKT Ruvu, Bakari Shime amesema wapo tayari kwa Ligi Daraja la Kwanza wapambane kurejea Ligi Kuu 

    JKT Oljoro itaanza kampeni ya kuwania kurudi Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuwafuata Transit Camp mkoani Shinyanga katika mchezo wa ufunguzi wa ligi hiyo.
    “Kikosi changu kitaondoka hapa (Arusha) Alhamisi wiki hii hapa kwenda Shinyanga kwa ajili ya mchezo huo. Ninawaomba wapenzi wa soka wa mkoa wa Arusha na maeneo  
    ya jirani waisapoti timu hii ili iweze kurejea Ligi Kuu msimu ujao,”amesema Massawe.
    Wakati huo huo: Timu nyingine ya Jeshi la Kujenga Taifa, JKT Ruvu iliyoteremka Daraja msimu uliopita nayo imesema ipo tayari kupambana katika Ligi Daraja la Kwanza msimu huu.
    Kocha wa JKT Ruvu, Bakari Shime amesema kwamba wamefanya maandalizi ya kutosha na hivi sasa wapo tayari kwa michuano hiyo iliyopangwa kuanza Septemba 16, mwaka huu.
    JKT Ruvu ipo Kundi A na itanza kucheza na ndugu zao, Mgambo JKT Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
    Shime amesema mechi zao za nyumbani watacheza kwenye Uwanja wao wa Mbweni JKT nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: JKT OLJORO, RUVU ZAPANIA KUPAMBANA DARAJA LA KWANZA ZIRUDI LIGI KUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top