• HABARI MPYA

    Sunday, September 10, 2017

    HAJJI MANARA ANAPASWA KUBADILIKA, ANAKOELEKEA ANAPOTOKA

    MAPEMA wiki hii kuliibuka malumbano kidogo, mashabiki wa Yanga wakimtukana na kumdhalilisha Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu ya Simba, Hajji Sunday Manara kwenye mitandao ya kijamii.
    Hasira za mashabiki wa Yanga zilifuatia Manara kuposti picha za kumdhalilisha mchezaji mpya wa mahasimu wao, Papy Kabamba Tshishimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). 
    Kweli Hajji aliposti maudhi kwa wana Yanga na udhalilishaji kwa kijana mwenzake, mwanaume mwenzake, mdogo wake, Kabamba Tshishimbi ambaye kaja Tanzania kama Emmanuel Okwi au Daniel Agyei kutafuta maisha na si kudhalilishwa.
    Lakini mashabiki wa Yanga nao walikosea kumrudi Hajji kwa matusi mazito ya jazba na mbaya zaidi kumdhalilisha kwa ulemavu wake wa ngozi. Mashabiki wanakemewa na sisi watu wa vyombo vya Habari na mimi natumia fursa hii kuwaambia mashabiki wa Yanga walikosea kumdhalilisha Hajji kwa ngozi yake.
    Yanga ina shabiki mlemavu wa miguu, mlemavu wa macho, mlemavu wa ngozi na hata mlemavu wa akili, hivyo kumdhalilisha Hajji kwa ngozi yake ieleweke imewagusa na kuwaumiza hata mashabiki wengine wa timu hiyo hiyo ya Jangwani.
    Lakini mashabiki ni mashabiki tu dunia nzima, wengi wao ni ‘wehu’ na wanaweza kufanya lolote lenye madhara na imeshuhudiwa hata kwenye michuano mikubwa duniani kama Euro, AFCON na Kombe la Dunia wakifanya vurugu kubwa na kusababisha athari kubwa kadhalika.
    Hapa nyumbani tu mashabiki wa Simba Oktoba 1, mwaka jana walivunja viti Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam wakati wa mchezo dhidi ya mahasimu wao, Yanga. Lakini mara nyingi mashabiki hawa huwa hawafanyi hivi hivi, lazima wanakuwa wana sababu na Oktoba 1, mwaka jana walikerwa na maamuzi ya utata ya refa Martin Saanya aliyechezesha mechi hiyo ya watani wa jadi.
    Wazi maamuzi ya utata ya Saanya yalikuwa chanzo za vurugu za Oktoba 1, mwaka jana baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.
    Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
    Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Nahodha wa Simba SC, Jonas Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele.
    Kwa hali hiyo, mchezo ukasimama kwa takriban dakika tano baada ya mashabiki wa Simba kuanza kufanya vurugu waking’oa viti na kutupa uwanjani. Polisi walitumia milipuko ya gesi za kutoa machozi kuwatuliza mashabiki hao na mchezo ukaendelea hadi Simba SC wakasawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shiza Kichuya.
    Baadaye pamoja na kuwafungia waamuzi huo miaka miwili kwa makosa ya kutoa maamuzi ya utata, pia Kamati ya Masaa 72 ya Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilifuta Kadi nyekundu ya mchezaji Jonas Mkude baada ya kubaini hakufanya kosa.
    Na vurugu za mashabiki wa Yanga wiki hii zilisababishwa na Hajji mwenyewe kuposti picha za kumdhalilisha mchezaji wa mahasimu wao. Mambo yanapotokea hata yasipotuachia athari zozote, lakini huwa yanaacha fundisho – basi vyema Hajji naye akajifundisha baada ya hili la wiki hii, lakini kwanza akubali alifanya kosa.
    Watu wa Kongo utamaduni wao ni kujipenda na kujiremba kama wanawake na ndiyo wanaojulikana zaidi kwa utanashati hapa mjini kiasi kwamba hata kijana wa Kitanzania akivaa vizuri sana ataambiwa umevaa Kipapaa, sababu ndugu zetu hao wanatufundisha kupendeza.
    Vijana wa Kikongo wanatumia vipodozi vya kuwang’arisha ngozi hadi vijana wa Kitanzania wanaiga, wanajiremba kwa vipini vya pua na masikio na sasa wamehamia kwenye fasheni ya vikorokoro vingine jamii ya bangili za miguu na mikono ambavyo ni maarufu kwa wanawake. 
    Hiyo ndiyo asili yao Wakongo na wako huru nayo popote waendako na tunapaswa kuwaheshimu kwa hilo kwa sababu muda si mrefu watoto wa mjini Dar es Salaam ambao tayari wanasuka nywele, kuvaa vipini, vya pua na masikio kama dada zao wataiga kuvaa na hivyo vipupu.
    Lakini kitu kimoja kikubwa ni kwamba, Hajji ni kiongozi hapaswi kufanya kitu alichokifanya, baadhi ya mambo anapaswa kuwaachia mashabiki wafanye, ili yeye aibuke kukemea hata kinafiki.
    Kuna mambo Hajji anahitaji kubadilika katika staili yake ya Usemaji wa klabu, bado yupo kizamani mno, enzi zile za kupiga kelele na kujenga chuki na uhasama – tumekwishatoka huko na ndiyo maana mashabiki wa Yanga walijichangisha fedha mwaka jana yeye akatibiwe macho India.
    Hajji anapaswa kujifunza kwa Ofisa Habari mpya wa Yanga, Dissmas Ten, jamaa anafanya kazi jinsi inavyotakiwa na inaonekana. Si mpayukaji. Yanga taratibu wamekwishazoea hali mpya – mambo yanashughulikiwa, watu hawapigi kelele tu kwenye vyombo vya habari kutafuta sifa na umaarufu.
    Hajji anapayuka kwenye vyombo vya Habari, Emmanuel Okwi anakuja, kumbe klabu haijamtumia tiketi kutoka Misri amekwenda Uganda ndiyo apate usafiri mwingine wa kuja Dar e Salaam matokeo yake amekosa mechi muhimu jana dhidi ya Azam FC.   
    Naona kama nataka kutoka nje ya mada – lengo ni kumshauri Msemaji wa Simba, Hajji Sunday Manara abadilike, yeye kama kiongozi anapaswa kuwaheshimu wachezaji na si kuwadhalilisha kama alivyofanya kwa Tshishimbi. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAJJI MANARA ANAPASWA KUBADILIKA, ANAKOELEKEA ANAPOTOKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top