• HABARI MPYA

    Sunday, September 10, 2017

    HAJIB AWAPA RAHA YANGA...AFUNGA BAO PEKEE NJOMBE YAFA 1-0 SABA SABA

    Na Rehema Lucas, NJOMBE
    MABINGWA watetezi, Yanga SC leo wamevuna pointi tatu za kwanza katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bada baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Njombe Mji Uwanja wa Saba Saba mjini Njombe.
    Shukurani kwake, mshambuliaji mpya, Ibrahim Hajib Migomba aliyefunga bao hilo pekee kipindi cha kwanza na sasa Yanga inafikisha pointi nne baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Lipuli ya Iringa kwenye mchezo wa kwanza nyumbani, Dar es Salaam. 
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Suleiman Kinugani wa Morogoro, aliyesaidiwa na Khalfan Sika wa Pwani na Hajji Mwalukuta wa Tanga, Hajib alifunga bao hilo dakika ya 16 kwa shuti la umbali wa mita 30 la mpira wa adhabu, baada ya yeye mwenyewe kuangushwa.
    Ibrahim Hajib (kushoto) leo amefunga bao pekee Yanga ikishinda 1-0 Njombe
    Yanga waliongeza kasi ya mashambulizi baada ya bao hilo, lakini hawakuwa na bahati ya kufunga zaidi kutokana na kushindwa kutumia vizuri nafasi walizotengeneza.
    Kwa ujumla Yanga SC walitawala vizuri mchezo kipindi chote cha kwanza na wangeweza kuvuna mabao zaidi kama wangekuwa makini katika utumiaji wa nafasi.
    Kipindi cha pili kilibadilika kidogo na vijana wa Hassan Banyai wakaanza kuwavimbia mabingwa watetezi wa Ligi Kuu walio chini ya kocha Mzambia, George Lwandamina.
    Sifa zimuendee kipa Mcameroon wa Yanga, Youthe Rostand aliyeokoa michomo mingi ya hatari kipindi hicho cha pili na kuinusuru timu yake kufungwa.
    Katika kipindi hicho, beki wa Njombe Mji, Remmy Mbuligwe alikimbizwa hospitali baada ya kuumia kufuatia kugongana na beki wa Yanga Juma Abdul.
    Awali ya hapo, Yanga nayo ilipata pigo baada ya kiungo wake Mzimbabwe, Thabani Kamusoko kuumia na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Raphael Daudi dakika ya 49.     
    Katika mechi nyingine za leo; Lipuli FC imeilaza 1- 0 Stand United, Mbeya City imefungwa nyumbani 1-0 na Ndanda FC, Singida United imeifunga 2-1 Mbao FC, Kagera Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar imeshinda 1-0 dhidi ya FC Mwadui.
    Kikosi cha Njombe Mji kilikuwa; David Kisu, Agaton Mapunda, Remmy Mbuligwe, Laban Kamboole, Peter Mwangosi, Joshua John, Awadh Salum, Hassan Kapalata/Behewa Sembwana dk80, Notikeli Masasi, Ditrim Nchimbi na David Nakpa/Raphael Siame dk47.
    Yanga SC; Youthe Rostand, Juma Abdul, Gardiel Michael, Andrew Vincent, Kevin Yondan, Papy Kabamba Tshishimbi, Juma Mahadhi, Thabani Kamusoko/Raphael Daudi dk49, Donald Ngoma/Obrey Chirwa dk56, Ibrahim Hajib na Emmanuel Martin/Yussuf Mhilu dk70. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAJIB AWAPA RAHA YANGA...AFUNGA BAO PEKEE NJOMBE YAFA 1-0 SABA SABA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top