• HABARI MPYA

    Saturday, September 09, 2017

    DOGO WA SERENGETI BOYS AFUZU MAJARIBIO ETOILE DU SAHEL YA TUNISIA

    Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
    MSHAMBULIAJI chipukizi wa Tanzania, Yohana Oscar Nkomola amefuzu majaribio katika klabu ya Etoile Du Sahel ya Tunisia na sasa anatarajiwa kusaini mkataba.
    Akizungumza mjini Dar es Salaam leo baada ya kuwasili kutoka Tunisia, kufuatia majaribio ya wiki tatu, Nkomola amesema kwamba anamshukuru Mungu kwa mafanikio hayo, kwani hizo ndizo ndoto zake.
    “Ninamshukuru Mungu kwa kuniwezesha kupata nafasi hii na ninaamini huu ni mwanzo mzuri kwangu kuelekea kutimiza ndoto zangu za kuwa mchezaji mkubwa,”amesema.
    Hata hivyo, Nkomola amesema atatakiwa kuchezea timu ya vijana hadi April mwakani atakapofikisha umri wa miaka 18 ndipo asaini mkataba na kuanza kuchezea timu ya wakubwa.
    Yohanna Nkomola (kushoto) akiwa na wenzake baada ya kurejea leo mjini Dar es Salaam
    “Nimerudi hapa nyumbani kukamilisha taratibu fulani, baada ya wiki mbili nitaondoka kurejea Tunisia ambako nikifika kwanza nitaanza kuchezea timu B ya vijana hadi nifikishe umri wa miaka 18 mwezi wa nne (2018) ndipo nisaini mkataba na kuanza kuchezea timu ya wakubwa,”amesema.
    Nkomola alikwenda Tunisia pamoja na wachezaji wengine wawili aliokuwa nao timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki Fainali za Vijana Afrika Mei mwaka huu nchini Gabon, Ally Ng’anzi na Eric Nkosi.  
    Bahati mbaya kwa Ng’anzi na Nkosi hawakufuzu majaribio na wanarejea nyumbani kuendelea na harakati za kujiinua kisoka.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: DOGO WA SERENGETI BOYS AFUZU MAJARIBIO ETOILE DU SAHEL YA TUNISIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top