• HABARI MPYA

    Saturday, August 19, 2017

    KAGERA SUGAR YABARIKI MBARAKA YUSSUF KUCHEZA AZAM FC

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa Azam FC na ule wa Kagera Sugar jana ulifikia muafaka kuhusu usajili wa mshambuliaji Mbaraka Yussuf.
    Baada ya klabu hizo kukaa mezani, sasa Kagera Sugar imemruhusu rasmi mshambuliaji wake huyo wa zamani kukipiga kwa mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii msimu uliopita.
    Awali uongozi wa Kagera Sugar, ulimwekea pingamizi mshambuliaji huyo wakidai bado ana mkataba wa miaka mitatu ndani ya kikosi hicho, jambo ambalo zilizifanya pande zote mbili kukutana na kufikia muafaka.
    Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, amesema kwamba baada ya makubaliano hayo uongozi wa Kagera Sugar umeamua kwenda kuliondoa pingamizi waliloenda kumwekea Yussuf kwenye Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Kagera Sugar imebariki usajili wa Mbaraka Yussuf Azam FC

    “Baada ya mazungumzo ya muda mrefu kila kati ya Kagera na Azam lakini kila mmoja akivutia upande wake, hatimaye jana Kagera Sugar walikuja katika ofisi zetu za Azam na kuweza kufanya mazungumzo ya pamoja tunashukuru Mungu kwamba mazungumzo yamekwenda vizuri na utaratibu umekwenda vizuri.
    “Kila siku Azam FC tunasema kwamba michezo ni udugu na vile vile ni familia, kwa hiyo katika mazungumzo kati ya Azam FC na Kagera Sugar ni kwamba Kagera Sugar imemruhusu rasmi mchezaji Mbaraka Yussuf Abeid kuichezea klabu ya Azam FC,” alisema.
    Idd alisema kuwa mara baada ya klabu hiyo kuridhia, jana hiyo hiyo uongozi wa Kagera Sugar uliandika barua ya kumruhusu kuondoka (release letter), ambayo nakala moja imekwenda TFF, nyingine Azam FC na moja wamempa mchezaji huyo ikiwa ni kumruhusu na kwamba yuko huru kujiunga na mabingwa hao.
    “Kinachoendelea ni kwamba Kagera Sugar wamekwenda kutoa pingamizi lao dhidi ya Azam FC juu ya mchezaji Mbaraka Yussuf baada ya mazungumzo ya jana kwenda vizuri, tunashukuru Mungu kuwa suala hili limekwenda vizuri, na tunawaambia masha biki wa Azam FC wasiwe na wasiwasi, Mbaraka Yussuf kwa sasa yupo Azam FC na amepata baraka zote za Kagera Sugar,” alisema.
    Wakati huo huo, Idd alisema kuwa mshambuliaji Shaaban Idd, aliyetakiwa kuondoka jana nchini kwenda Afrika Kusini kwa uchunguzi wa tatizo la misuli ya nyama za paja inayomsumbua, sasa ataondoka leo Jumamosi akiwa sambamba na Meneja Mkuu, Abdul Mohamed, tayari kabisa kwa matibabu yake.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAGERA SUGAR YABARIKI MBARAKA YUSSUF KUCHEZA AZAM FC Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top