• HABARI MPYA

    Thursday, August 17, 2017

    AZAM YAWASUTA KAGERA SUGAR, YASEMA IMEFUATA TARATIBU ZOTE KUMSAJILI MBARAKA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    UONGOZI wa Azam FC umewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuhusu usajili wa mshambuliaji Mbaraka Yussuf, aliyewekewa pingamizi na timu yake ya zamani ya Kagera Sugar.
    Azam FC imefanikiwa kumsajili Mchezaji huyo Bora Chipukizi wa VPL msimu uliopita kwenye usajili huu, kwa mkataba wa miaka miwili na tayari ameungana na kikosi hicho kilichomaliza kambi yake ya siku 10 nchini Uganda juzi kujiandaa na msimu ujao.
    Kagera Sugar inadai bado ina mkataba na mchezaji huyo wa miaka mitatu, ikipeleka pingamizi hilo la usajili kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ambayo inatarajia kukutana Jumapili hii kupitisha usajili.
    Taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffar Idd, leo imeeleza kuwa timu hiyo ilimsajili mchezaji huyo kwa kufuata taratibu zote za usajili, huku akidokeza kuwa tayari Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limeidhinisha usajili wake kupitia mfumo mpya wa usajili wa kimtandao wa TMS.
    “Kagera Sugar ni timu ya muda mrefu kwenye ligi toka ipande haijawahi kushuka, Kagera Sugar wao wanalalamika kuwa Azam FC imemsajili mchezaji wao ambaye ni Mbaraka Yusuph Abeid, wakidai bado ana mkataba wa miaka mitatu.
    Azam FC imesema imefuata taratibu zote kumsajili Mbaraka Yussuf 

    “Lakini sisi kama Azam FC, uongozi baada ya kuamua kumsajili mchezaji huyo ni kwamba tumefuata taratibu zote na tumeona kuwa mkataba wake umekwisha na yupo huru na mkataba wa mwaka mmoja wa mchezaji huyo alioingia na Kagera Sugar umekwisha Juni 19, kwa hiyo tayari alishakuwa mchezaji huru,” alisema.
    Idd alisema kuwa kwa Azam FC kuamua kumsajili walipitia vigezo vyote na kuamini kabisa alikuwa ni mchezaji huru na ataweza kuichezea Azam FC msimu ujao.
    “Kingine kabisa Azam FC iliamua kupeleka jina la Mbaraka Yusuph kwenye usajili huu kwa maana kwenye TMS, na jina lake limerudi vizuri limekubalika na FIFA baada ya kufanya usajili kupitia TMS, wenzetu wa Kagera Sugar wao jina la Mbaraka hawakupeleka.
    “Hiyo inaonyesha kuwa tayari Kagera Sugar wameshakubali kuwa mchezaji huyo mkataba wanaosema kuwa wa miaka mitatu si wa kweli na wa kweli ni wa mwaka mmoja ulioisha, ni kweli kabisa Kagera Sugar ni wenzetu na kwenye mpira ni marafiki zetu, kama kweli walikuwa na mkataba wa miaka mitatu basi lazima na wao wangepeleka jina, kwa hiyo majina mawili yangepelekwa kwenye TMS.
    “Na kwenye TMS yakienda majina mawili basi ni kwamba inakataa usajili na inarudisha kwa TFF kutaka ukweli kutambua kuwa mchezaji huyu sasa hivi yuko wapi, Azam FC tunamatumaini mchezaji huyu tutampata ila hatuna ugomvi na Kagera Sugar wala visasi na Kagera Sugar isipokuwa lazima kanuni za mpira zifuatwe,” alisema
    Alimalizia kwa kusema kuwa, Azam FC ni moja ya timu zilizoandikiwa barua kufika kwenye kamati hiyo inayosshughulika na mambo ya usajili na kudai kuwa watakwenda Jumapili hiyo na vielelezo vyote vinavyostahiki na wakiwa na imani kuwa suala hilo litakwisha.
    Yussuf kwa sasa anaendelea na mazoezi mepesi tayari kabisa kurejea dimbani baada ya kufanyiwa upasuaji wa ngiri mwezi mwezi uliopita.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM YAWASUTA KAGERA SUGAR, YASEMA IMEFUATA TARATIBU ZOTE KUMSAJILI MBARAKA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top