• HABARI MPYA

    Monday, August 14, 2017

    AZAM FC YAENDELEZA 'MAUWAJI' MECHI ZA KIRAFIKI ZIARA YA UGANDA

    Na Mwandishi Wetu, KAMPALA
    TIMU ya Azam FC, jana jioni iliendeleza wimbil la ushindi kwenye mechi zake za kujiandaa na msimu katika kambi yake nchini Uganda baada kuichapa Onduparaka mabao 3-0.
    Huo ulikuwa ni mchezo wa nne wa kirafiki wa Azam FC nchini humo, baada ya awali kutoka sare mbili, na Ijumaa iliyopita kuifunga URA mabao 2-0.
    Mabao ya Azam FC katika mchezo huo uliokuwa mkali na aina yake yamefungwa kiufundi na washambuliaji Yahaya Mohammed dakika ya 40, Yahya Zayd, dakika ya 63 kabla ya beki wa kulia Swaleh Abdallah, kupigilia msumari wa mwisho dakika ya 74, likiwa ni bao lake la kwanza tokea arejee Azam FC akitokea Majimaji kwa usajili wa miaka miwili.
    Yahya Mohammed amefikisha mabao manne katika ziara ya Azam FC nchini Uganda

    Bao alilofunga leo Yahaya limemfanya kufikisha mabao manne kwenye mechi tisa za Azam FC za maandalizi ya msimu ujao walizocheza mpaka sasa, akifunga moja wakati timu hiyo ilipofungwa na Rayon Sports mabao 4-2.
    Akafunga tena mawili wakati Azam FC ikiichapa URA 2-0 juzi kwenye Uwanja wa Phillip Omondi, kabla ya leo kutupia jingine, huku kinda Yahya Zayd, naye akiwa ametupia mawili katika mechi hizo za maandalizi.
    Jambo la kuvutia zaidi kwenye mechi zote za maandalizi za timu hiyo nchini Uganda, Azam FC imeendelea kuonyesha kandanda safi la pasi na mpira wa kasi huku wachezaji wapya wakionekana kuingia haraka kwenye mifumo.
    Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itamalizia kambi yake ya maandalizi nchini Uganda kwa kucheza mtanange wa mwisho kesho Jumatatu dhidi ya Vipers, utakaofanyika Uwanja wa St. Marys unaotumiwa na timu hiyo, uliopo Kitende nchini humo.
    Kikosi hicho kitaanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam, keshokutwa Jumanne, tayari kabisa kwa kumalizia maandalizi ya mwisho kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaoanza rasmi Agosti 26 mwaka huu, Azam FC ikiwa imepangiwa kuanzia ugenini kwa kukipiga na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
    Kikosi cha Azam FC jana kilikuwa; Razak Abalora, Himid Mao/Idd Kipagwile dk 89, Bruce Kangwa, Aggrey Morris, Yakubu Mohammed, Daniel Amoah, Stephan Kingue/Masoud Abdallah, Frank Domayo/Salmin Hoza dk 87, Salum Abubakar/Swaleh Abdallah dk 55, Yahya Zayd/Joseph Kimwaga dk 81, Yahaya Mohammed/Braison Raphael dk 62
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM FC YAENDELEZA 'MAUWAJI' MECHI ZA KIRAFIKI ZIARA YA UGANDA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top