• HABARI MPYA

    Friday, July 07, 2017

    TAIFA STARS WABEBA DOLA 10,000 COSAFA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    TANZANIA imefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika michuano ya COSAFA Castle baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku huu Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
    Shujaa wa Taifa Stars leo amekuwa golikipa Said Mohammed Mduda aliyepangua penalti ya Nahodha wa Mamba, Thapelo Mokhehle baada ya Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.
    Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao,Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.
    Nahodha wa Tanzania, Himid Mao (kulia) akiweka mpira kifuani mbele ya kiungo wa Lesotho, Napo Matsoso (kushoto) leo Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini

    Kipa Said Mohammed amepangua penalti ya Nahodha wa Lesotho, Thapelo Mokhehle kuipa Tanzania ushindi wa tatu COSAFA
    Ushindi unakuja siku 25 baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 Juni 10, mwaka huu katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Romeo Kasengele wa Zambia, aliyesaidiwa na washika vibendera Thomas Kusosa wa Zimbabwe na Helder de Carvalho wa Angola, ndani ya dakika 90 timu hizo zilishambuliana kwa zamu, Lesotho wakitawala zaidi kipindi cha kwanza na cha pili Taifa Stars wakazinduka.
    Kutoka na ushindi huo, Tanzania inaondoka na dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300.
    Fainali ya COSAFA Castle 2017 itachezwa Jumapili Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg baina ya majirani, Zambia na Zimbabwe na bingwa atapata dola 42,000 na mshindi wa pili dola 21,000.
    Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Said Mohammed, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Nurdin Chona, Salim Mbonde/Abdi Banda dk61, Salmin Hoza/Muzamil Yassin dk61, Himid Mao, Simon Msuva, Raphael Daudi, Stahmili Mbonde/Elias Maguri dk71 na Shiza Kichuya.
    Lesotho; Samuel Ketsekile, Itumeleng Falene, Motlomelo Mkwanazi, Thapelo Mokhehle, Bokang Sello, Kefuce Mahula/ Hlompho Kalake dk89, Tumelo Khutlang, Tsoanelo Koetle, Napo Matsoso, Jane Ntso/ Mabuti Potloane dk59 na Sera Motebang.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS WABEBA DOLA 10,000 COSAFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top