• HABARI MPYA

    Sunday, July 09, 2017

    TAIFA STARS SASA INALETA MATUMAINI, VIJANA WASILEWE SIFA TU

    SOKA ya Tanzania imeanza kujiinua tena taratibu, baada ya anguko baya mwanzoni mwa muongo huu.
    Wakati Watanzania bado hawajasahau mafanikio ya timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kushiriki Fainali za Afrika na kuonyesha upinzani mwezi Mei mwaka huu nchini Gabon, wanapokea faraja nyingine.
    Hiyo si nyingine zaidi ya timu ya taifa ya wakubwa, chini ya benchi jipya kabisa la Ufundi kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA).
    Taifa Stars imefanikiwa kushika nafasi ya tatu katika Kombe la COSAFA Castle baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa Ijumaa Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
    Shujaa wa Taifa Stars siku hiyo alikuwa kipa wa Mtibwa Sugar, Said Mohammed Mduda aliyepangua penalti ya Nahodha wa Mamba, Thapelo Mokhehle baada ya Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.
    Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao, Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.
    Ushindi huo unakuja siku 25 baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 Juni 10, mwaka huu katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
    Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Romeo Kasengele wa Zambia, aliyesaidiwa na washika vibendera Thomas Kusosa wa Zimbabwe na Helder de Carvalho wa Angola, ndani ya dakika 90 timu hizo zilishambuliana kwa zamu, Lesotho wakitawala zaidi kipindi cha kwanza na cha pili Taifa Stars wakazinduka.
    Kutokana na ushindi huo, Tanzania imeondoka na dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300.
    Michuano ya COSAFA Castle mwaka huu inafikia tamati leo kwa mchezo wa fainali Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg baina ya majirani, Zambia na Zimbabwe na bingwa atapata dola 42,000 na mshindi wa pili dola 21,000.
    Tanzania imecheza jumla ya mechi sita ndani ya wastani wa siku 12 kwenye COSAFA, ikishinda tatu, sare mbili na kufungwa moja.   
    Ilianza kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Malawi, kabla ya kutoa sare ya 0-0 na Angola, 1-1 na Mauritius katika mechi za Kundi A hivyo kufanikiwa kwenda Robo Fainali, ambako iliwafunga wenyeji, Bafana Bafana 1-0 na kwenda Nusu Fainali, ilipofungwa na Zambia 4-2.
    Na Julai 7 katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu ikaichapa Lesotho kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 0-0 na kuchukua Medali ya Shaba ya COSAFA 2017.
    Matokeo haya ni mazuri katika mwanzo wa zama mpya za Taifa Stars, chini ya kocha Salum Mayanga anayesaidiwa na Fulgence Novatus na Patrick Mwangata.
    Kinacholeta matumaini si matokeo, bali uchezaji wa timu kuanzia wa mchezaji mmoja mmoja na kikosi kizima, kilichosheheni damu mpya na changa.
    Katika mechi ya mwisho, Nurdin Chona alicheza vizuri beki ya kati kwa pamoja na Salim Mbonde kwanza kabla ya kumalizia na Abdi Banda, wakati viungo Salmin Hozza na Raphael Daudi nao walianzishwa na wakacheza vizuri.
    Gardie Michael Mbaga amecheza mechi zote sita katika beki ya kushoto na amekuwa na mwanzo mzuri, kiasi kwamba Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akipona ajue ana mshindani wa namba sasa.
    Stahmili Mbonde alianzishwa kama mshambuliaji pekee katika mchezo wa mwisho na akaenda kuwashughulisha mabeki wa Lesotho, kabla ya dakika za mwishoni kabisa kumpisha Elias Maguri.
    Usisahau, Aishi Manula alisimama langoni kwenye mechi zote za mwanzo na akadaka vizuri, ingawa Mduda alionekana kumalizia vizuri zaidi michuano kwa kuiwezesha timu kushika nafasi ya tatu.
    Kipa wa tatu, Benno Kakolanya naye yuko vizuri japokuwa hakudaka hata mchezo mmoja – jambo linaloashiria kwamba nafasi hiyo ina ushindani unaompa changamoto kila mmoja wao kuhakikisha anakuwa vizuri na tayari wakati wote.
    Himid Mao, Muzamil Yassin, Shiza Kichuya, Simon Msuva ni wachezaji wengine vijana katika kikosi cha kwanza cha sasa cha Stars, ukiondoa mkongwe Erasto Nyoni.
    Mshambuliaji Mbaraka Yussuf Abeid alicheza mechi za mwanzo akitokea benchi, kabla ya kuugua na kushindwa kuendelea na mashindano. Elias Maguri, Thomas Ulimwengu, Shomary Kapombe ni wachezaji wakubwa na ambao wanaweza kuendelea kucheza kwa kiwango cha juu kwa miaka hata mitano ijayo wakijitunza.
    Pamoja na ambao hawakuwepo, akiwemo Nahodha Mbwana Samatta anayecheza KRC Genk ya Ubelgiji na Farid Mussa wa DC Tenerife B ya Hispania inapatikana picha nzuri ya Taifa Stars mpya.
    Taifa Stars ya zama mpya, ambayo inatarajiwa kuwapoza machungu Watanzania baada ya matokeo mbaya ya muda mrefu.
    Pongezi kwao kwa ushindi wa tatu COSAFA, lakini wasibweteke kwa sababu bado wana mitihani migumu mbele yao, kuwania tiketi za AFCON na CHAN. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: TAIFA STARS SASA INALETA MATUMAINI, VIJANA WASILEWE SIFA TU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top