• HABARI MPYA

  Saturday, July 08, 2017

  SOKA YA TANZANIA ‘YAHAMIA’ GEREZA LA KEKO

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  VIONGOZI wote wakuu wa klabu kubwa nchini pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wapo rumande gereza la Keko, Dar es Salaam.
  Aliyekuwa Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji alikuwa mtu wa mwisho kuingizwa kwenye gereza hilo juzi kuungana na Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu wake, Selestine Mwesigwa.
  Manji alijiuzulu Uenyekiti wa Yanga mwezi uliopita kutokana na kile alichosema sababu zilizo nje ya uwezo wake, ingawa tangu kumekuwa na juhudi za wanachama kumbembeleza arejee.  
  Manji alinyimwa dhamana juzi baada ya kusomewa mashitaka ya Uhujumu Uchumi, ikiwamo kukutwa na vitambaa vya sare za Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) akiwa amelazwa kitandani katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
  Wote wapo gerezani; Viongozi wa klabu za Simba na Yanga pamoja na TFF wapo rumande kwa tuhuma mbalimbali

  Hiyo ni baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kulazimika kuhamishia shughuli zake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuwasomea mashtaka ya uhujumu uchumi Manji mwenyee umri wa miaka (41) na wenzake.
  Manji na wenzake pia wanatuhumiwa kukutwa na mihuri ya mbalimbali ya JWTZ pasipo na uhalali, vyote vikiwa na thamani ya Sh. milioni 236.5.
  Mahakama hiyo ilifika viunga vya taasisi hiyo Saa 9:10 alasiri na moja kwa moja kuingia wadi namba moja alikolazwa Manji huku washtakiwa wenzake wakifikishwa na gari ya polisi aina ya Land Cruiser yenye namba za usajili T 968 DHS na kuungana na mtuhumiwa mwenzao.
  Mahakama hiyo iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, ilianza kusikiliza mashtaka ya Jamhuri saa 9:35 katika wodi hiyo.
  Upande wa Jamhuri uliongozwa na Mawakili wa Serikali Waandamizi, Nassoro Katuga, Mutalemwa Kishenyi na Tulumanywa Majigo huku, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Hudson Ndusyepo, Emmanuel Safari na Seni Malimi.
  Majigo aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni, Ofisa Rasilimaliwatu Deogratias Kisinda (28), Mtunza Stoo, Abdallah Sangey (46) na Mtunza Stoo msaidizi, Thobias Fwele (430
  Alidai katika shtaka la kwanza kuwa Juni 30, mwaka huu eneo la Chang'ombe Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Manji na wenzake walikutwa na askari polisi wakiwa na Mabunda (majola) 35 ya vitambaa vya vinavyotengezea sare za JWTZ zenye thamani ya Sh. milioni 192.5 na kwamba zilipztikana isivyo halali.
  Katika shitaka la pili, ilidaiwa kuwa mekutwa Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A' Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabando nane ya sare za JWTZ zenye thamani ya Sh. milioni 44.
  Upande huo wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa, Juni 30,mwaka huu eneo la tukio la kwanza, washtakiwa walikutwa na mhuri wa JWTZ uliokuwa na maandishi 'Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha Jeshi JWTZ' bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.
  Majigo aliendela kudai katika shtaka la nne, siku ya tukio la tatu, washtakiwa wote kwa pamoja walikuwa na mhuri wenye maandishi "Kamanda Kikosi 834 Kj Makutupora Dodoma" bila uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.
  Shitaka la tano, siku ya tukio la tatu na la nne, mshtakiwa alikutwa na mhuri wenye maandishi "Comanding Officer 835 Kj  Mgambo P.O BOX 224 Korogwe" bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha uslama wa nchi.
  Ilidaiwa katika shtaka la sita, Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A', washtakiwa wote walikutwa na pleti namba za gari zenye usajili wa SU 383 iliyopatikana isivyo halali.
  Majigo alidai katika shtaka la saba, eneo la tukio la sita, washtakiwa walikutwa na pleti namba za gari zenye namba ya usajili SM 8573 iliyopatikana isivyo halali.
  Kwa mujibu wa mashtaka hayo yaliyofunguliwa chini ya sheria ya uhujumu uchumi na usalama wa taifa, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao.
  Upande wa Jamhuri uliwasilisha hati ya kuzuia dhamana kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP), akiomba washtakiwa wasipewe dhamana kwa usalama wao na maslahi ya taifa.
  DPP pia alieleza sababu nyingine kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kushughulikia dhamana dhidi ya kesi hiyo.
  Hata hivyo, upande wa utetezi ulidai kuwa upande wa Jamhuri una nia mbaya kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana dhidi ya washtakiwa kuwasilisha hati hiyo ni kuwanyima haki.
  Hakimu Shaidi alisema upande wa utetezi wawasilishe hoja zao Mahakama Kuu yenye mamlaka ya kusikiliza kesi yao na kwamba hawezi kutoa amri yoyote chini ya mahakama yake.
  Alisema kesi hiyo itatajwa Julai 19, mwaka huu na washtakiwa watatu walipelekwa mahabusu ya Keko huku Manji akiwa chini ya ulinzi wa polisi wodini hapo wakati akisubiri askari magereza kupokea hati yake ya kuwa mahabusu.
  Mahakama hiyo ilimaliza shughuli zake saa 10.35 alasiri na wakati wote Manji alikuwa amelala kitandani huku washtakiwa wenzake wakiwa wamesimama wakati mashtaka yanasomwa.
  Awali ya hapo, Malinzi, pamoja na Katibu wa TFF, Selestine Mwesigwa na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Keko Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
  Walirudishwa Mahakamani Julai 3, ambako walinyimwa dhamana tena na kurejeshwa rumande hadi Julai 17, upepelezi wa kesi yao utakapokamilika.
  Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
  Katika kesi hiyo, Serikali inawakilishwa na jopo la mawakili watano, wakiongozwa na Pius Hila huku upande wa washtakiwa ukiwakilishwa na mawakili watano, wakiongozwa na Jerome Msemwa. Mawakili hao watano kwa pamoja wameshindwa kuafikiana ili washitakiwa wapatiwe dhamana.
  Aveva na Makamu wake, Kaburu nao Juni 29, mwaka huu walipelekwa mahabusu hadi Julai 13, mwaka huu baada ya kunyimwa dhamana kufuatia kusomewa mashitaka matano Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
  Wawili hao walifikishwa mahakamani mapema asubuhi ya siku hiyo na kusomewa mashitaka hayo matano mchana, ambayo ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodai kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni Rais Aveva na Makamu wake, Kaburu kiasi cha dola za Kimarekani 300,000.
  Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwenye benki ya CRDB tawi la Azikiwe mjini Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sharia, ambapo inadaiwa Rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
  Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka kwenye benki ya  Barclays tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu aliyemsadia Aveva kutakatisha fedha katika Barclays baada ya kughushi nyaraka.
  Baada ya kusomewa mashitaka hayo na wakili wa Serikali, Christopher Msigwa, washitakiwa hao walikana mashitaka yote na kupelekwa rumande hadi Julai 13, mwaka huu huku wakinyimwa dhamana.
  Wawili hao walipandishwa kizimbani jana baada ya juzi kukamatwa na Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa uchunguzi juu ya tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kutokana na mchezaji Emmanuel Okwi.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SOKA YA TANZANIA ‘YAHAMIA’ GEREZA LA KEKO Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top