• HABARI MPYA

  Tuesday, July 11, 2017

  SIMBA: BANDA ATAKWAMISHWA NA UBISHI WAKE MWENYEWE

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  SIMBA SC imesema kwamba Abdi Hassan Banda atajikwamisha mwenyewe kujiunga na Baroka FC ya Afrika Kusini kutokana na ubishi wake.
  Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari leo, Simba imesema Banda alishauriwa jana kuandika barua ya kuomba barua ya kuruhusiwa kuondoka, lakini akagoma.
  “Klabu ya Simba inapenda kutoa ufafanuzi kuhusiana na malalamiko ya mchezaji Abdi Banda ambaye alilalalamika jana kupitia vyombo vya habari, kuwa klabu imemkatalia kumpa barua ya kumuacha ilhali yeye amepata timu huko Afrika kusini na huku akiwa amemaliza mkataba wake,”. 
  “Ni kweli Banda amemaliza Mkataba na klabu, na jana alikuja ofisini kwetu kutaka barua hiyo, lakini akakumbushwa kuwa, ukiwa umemaliza Mkataba haupaswi kupewa barua hiyo, wanaoandikiwa barua hiyo ni waajiriwa ambao bado wana mikataba na labda kwa sababu yoyote ile, klabu inaamua kuachana nao,”. 
  Abdi Banda wa pili kushoto akiwa na mabeki wenzake wa Taifa Stars, Shomary kapombe na Salim Mbonde kulia na Gardiel Michael kushoto
  “Lakini kwa kuwa Banda aliitaka hiyo barua, akaambiwa aandike barua fupi tu ya kuomba barua ya kuruhusiwa, ili ibaki kwenye kumbukumbu za klabu, lakini kwa mshangao wa Maafisa wa klabu aligoma kuiandikia barua klabu na kuamua kukimbilia kwenye vyombo vya habari,” imesema taarifa ya Simba. 
  Taarifa hiyo imeendelea kusema kwamba Simba imesikitishwa sana na kitendo hicho kinachojirudia cha kutafuta mchezaji huyo huruma kupitia vyombo vya Habari, huku akijua kuwa anaikosea heshima klabu na kuipaka matope bila sababu. 
  “Simba inaamini sana utamaduni wake wa miaka mingi wa kuwaruhusu wachezaji wake kwenda nje ya nchi kucheza soka pindi wapatapo nafasi hiyo, lakini inasisitiza sana suala la utaratibu, haijawahi kutokea kokote duniani, mchezaji aliyemaliza mkataba kudai barua ya kuruhusiwa, na k wa kweli tumeshangazwa pia na baadhi ya vyombo vya habari kulishupalia jambo hilo bila hata kutusikiliza,”
  “Na kwa kupitia barua hii, klabu inawaambia haitafanya kazi kwa shinikizo la mtu au chombo chochote kile, huku tukifahamu ni kinyume na utaratibu na utamaduni wa mchezo huu unaopendwa duniani kote,”imesema taarifa hiyo. 
  Simba pia imesema kwamba kuanzia sasa wataweka udhibiti mkubwa kwa wachezaji wake na benchi la ufundi kuongea na vyombo vya habari, huku pia ikisisitiza Banda akitaka barua ni wajibu wake kuandika barua pia, vinginevyo klabu inamtakia mafanikio makubwa huko aendako. 
  Banda amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Baroka ya Ligi Kuu wiki iliyopita baada ya kung’ara katika michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini akiiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu.
  Lakini baada ya kurejea nyumbani jana kushughulikia vibali na kukamilisha taratibu mbalimbali za uhamisho wake, amekutana na vikwazo.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: SIMBA: BANDA ATAKWAMISHWA NA UBISHI WAKE MWENYEWE Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top