• HABARI MPYA

    Wednesday, July 12, 2017

    ROONEY, EVERTON WAWASILI DAR TAYARI KWA ‘SHOW LA KESHO’ TAIFA

    Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
    KIKOSI cha wachezaji 25 wa Everton kimewasili mjini Dar es Salaam asubuhi ya leo tayari kwa mchezo maalum wa kirafiki na Gor Mahia ya Kenya kesho Uwanja wa Taifa, lakini kiungo Ross Barkley hayumo baada ya kuachwa kutokana na kuwa majeruhi.
    Everton imesema kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23 anasumbuliwa na maumivu ya nyonga na hayumo katika orodha ya nyota 25 waliotua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
    Miongoni mwa nyota waliowasili asubuhi ya leo na kupokewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe baada ya safari ya tangu usiku wa jana walipoondoka Uwanja wa Ndege wa Liverpool, ni wachezaji mpya Wayne Rooney, Michael Keane na Davy Klaassen.
    Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe akisalimiana na mchezaji wa Everton, Wayne Rooney baada ya kuwasilia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam asubuhi ya leo
    Barkley anaingia katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake, lakini hatasaini mkataba mpya na kocha wa Everton, Ronald Koeman anaamini Barkley atauzwa kama hatasaini, kwani umuhimu wake umepungua baada ya kuwasili kwa Rooney na Klaassen, pamoja na Gylfi Sigurdsson — wachezaji wote ambao wanaweza kucheza nafasi yake.
    Wachezaji waliowasili ni Jordan Pickford, Sandro Ramirez, Wayne Rooney, Kevin Mirallas, Aaron Lennon, James McCarthy, Idrissa Gana Gueye, Gareth Barry, Davy Klaassen, Muhamed Besic, Maarten Stekelenburg, Morgan Schneiderlin, Leighton Baines, Michael Keane, Ashley Williams, Phil Jagielka, Yannick Bolasie, Seamus Coleman, Ramiro Funes Mori, Tom Davies, Dominic Calvert-Lewin, Mason Holgate, Ademola Lookman, Joel Robles, Oumar Niasse, Matthew Pennington, Jonjoe Kenny na Joe Williams. 
    Mchezo huo utakaoanza Saa 11:00 jioni, utachezeshwa na refa maarufu nchini, Israel Mujuni Nkongo, wakati mgeni Rasmi atakuwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan.
    Gor Mahia ilipata nafasi ya kucheza na Everton baada ya kuibuka bingwa wa michuano ya SportPesa Super Cup, ikiwafunga mahasimu, AFC Leopards 3-0 katika fainali ya timu za Kenya tupu baada ya timu za wenyeji zote, Simba, Yanga na Singida United kutolewa mapema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ROONEY, EVERTON WAWASILI DAR TAYARI KWA ‘SHOW LA KESHO’ TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top