• HABARI MPYA

  Friday, July 07, 2017

  NI STARS AU MAMBA LA LESOTHO MSHINDI WA TATU COSAFA LEO?

  Na Mwandishi Wetu, RUSTERNBURG
  TIMU za taifa za Lesotho na Tanzania zitakutana katika mchezo wa kusaka nafasi ya tatu Kombe la COSAFA Castle kuanzia Saa 3:30 usiku leo Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
  Hiyo inafuatia timu hizo kutolewa katika Nusu Fainali juzi, Taifa Stars ikichapwa 4-2 na Zambia na Mamba wakipigwa 4-3 na Zimbabwe.
  Huo utakuwa mchezo wa marudiano ndani ya kipindi cha siku 26, baada ya Juni 10 timu hizo kukutana katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika na kugawana pointi kwa sare ya 1-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
  Nahodha wa Tanzania, Himid Mao Mkami ataiongoza timu leo kuwania nafasi ya tatu COSAFA

  Lesotho waliamini hawakushinda kwa sababu walikuwa ugenini, lakini Nahodha wa Tanzania, Mbwana Samatta ambaye hayupo kwenye michuano ya COSAFA, alisema Uwanja wa mdogo wa Chamazi uliwafanya washindwe kucheza katika ubora wao.
  Visingizio vyote hivyo kesho havitakuwapo, timu zote zitakutana katika Uwanja wa ugenini usiohusiana nao kabisa na ni mkubwa wa kutosha.
  Mchezo huo ni kipimo kizuri kwa timu zote kabla ya kurejea nchini mwao kuanza kampeni za kuwania tiketi ya Michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), Tanzania ikicheza na Rwanda Julai 14 mjini Mwanza na Lesotho ikianzia ugenini na Comoro. 
  Fainali ya COSAFA 2017 itapigwa Jumapili Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg baina ya majirani, Zambia na Zimbabwe.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: NI STARS AU MAMBA LA LESOTHO MSHINDI WA TATU COSAFA LEO? Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top