• HABARI MPYA

    Thursday, July 13, 2017

    MWAMBUSI AONDOKA YANGA ‘KIROHO SAFI’ NA HATAKI KUFUNDISHA POPOTE MSIMU HUU

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KOCHA Juma Mwambusi amesema kwamba hatafundisha timu yoyote msimu huu kufuatia kuondoka Yanga baada ya kumaliza mkataba wake.
    Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Mwambusi amesema kwamba dhamira yake ni kujiondoa kwenye shughuli za mpira kwa muda ili ashughulikie mambo yake mengine binafsi.
    Mwalimu huyo wa zamani wa Moro United, Prisons na Mbeya City, amesistiza kwa ushawishi wowote hata wa fedha ikitokea timu inataka kumrudisha kwenye mpira msimu huu, atashikilia msimamo wake wa kupumzika.
    “Mimi nimemaliza mkataba Yanga na sijaongeza, kwa sababu dhamira yangu ya muda mrefu ni kupumzika kwa msimu huu ili nifanye mambo yangu binafsi,”amesema.
    Juma Mwambusi hatafundisha timu yoyote msimu huu kufuatia kuondoka Yanga baada ya kumaliza mkataba wake

    Mwambusi amesema msimu ujao atarejea kwenye mpira baada ya kukamilisha jukumu analotaka kulifanya kwa sasa.
    Mwambusi amefanya kazi Yanga kwa misimu miwili kama kocha Msaidizi, kwanza chini ya Mholanzi, Hans van der Pluijm na baadaye Mzambia, George Lwandamina aliye kazini kwa sasa. 
    Kocha huyo Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013/2014 akiwa na Mbeya City ya nyumbani kwao, Mbeya alifanya kazi kwa maelewano mazuri na ‘wakubwa’ zake wote, Pluijm na Lwandamina.
    Na Bin Zubeiry Sports – Online inaamini Yanga inaachana na Mwambusi tu kwa sababu za kuyumba kiuchumi, kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili wake, Yussuf Manji.
    Kwa sasa anayekaimu Ukocha Msaidizi wa Yanga ni beki na Nahodha wa zamani wa timu hiyo, Nsajigwa Shadrack Joel Mwandemele, aliyekuwa kocha wa kikosi cha vijana cha wana Jangwani hao.
    Juma Mwambusi (kulia) alianza kama Msaidizi wa Hans van der Pluijm Yanga

    Akamaliza kama Msaidizi wa Mzambia George Lwandamina, ambaye anamuacha kazini kwa sasa
    Lakini habari zaidi zinasema Yanga inataka kumchukua kocha wa Kagera Sugar, Mecky Mexime kuwa Mwalimu Msaidizi wa kikosi cha kwanza na Nsajigwa aendelee na kazi ya kutengeneza vipaji Yanga B.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MWAMBUSI AONDOKA YANGA ‘KIROHO SAFI’ NA HATAKI KUFUNDISHA POPOTE MSIMU HUU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top