• HABARI MPYA

  Friday, July 14, 2017

  MHADHIRI VYUO VYA ULAYA AWA KATIBU MKUU SIMBA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KLABU ya Simba imemteua Dk. Arnold Kashembe kuwa katibu Mkuu mpya, akichukua nafasi ya Patrick Kahemele aliyeondoka mwanzoni mwa mwaka, baada ya kufanya kazi miezi nane tu.
  Taarifa ya Simba imesema kwamba uteuzi huo umefanyika baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya klabu kilichofanyika jana jioni hoteli ya Serena, Dar es Salaam chini ya Kaimu Rais, Salim Abdallah Muhene ‘Try Again’ na Kaimu Makamu wake, Iddi Kajuna.
  Taarifa ya Simba imesema uteuzi wa msomi huyo mwenye shahada ya Uzamivu na aliyekuwa Mhadhiri kwenye Vyuo Vikuu mbalimbali Ulaya, unaanza mara moja. 
  Dk. Arnold Kashembe ndiye Katibu Mkuu mpya wa Simba, anachukua nafasi ya Patrick Kahemele aliyeondoka mwanzoni mwa mwaka 

  Pamoja na hayo, taarifa hiyo imesema kwamba kikao kimeitisha Mkutano mkuu wa kawaida utakaofanyika Agosti 13, mwaka huu ukifuatiwa na mkutano Mkuu wa kujadili mabadiliko ya Katiba, Agosti 20, mwaka huu.
  “Mikutano hiyo imeitishwa kwa kuzingatia matakwa ya katiba ya klabu, yanayotaka notisi ya kuitishwa mikutano hiyo ifanywe siyo chini ya siku thelathini kabla ya mikutano yenyewe,”imesema taarifa hiyo. 
  Taarifa hiyo pia imewataka wanachama na mashabiki wake kuendelea kuwa watulivu, hususan kipindi hiki ambacho viongozi wakuu, Rais Evans Elieza Aveva na Makamu wake, Geofffrey Nyange ‘Kaburu’ wako rumande kwa mashitaka matano dhidi ya Serikali.
  Aveva na Kaburu jana walipandishwa mahakamani kwa mara ya tatu na kesi yao kuahirishwa tena hadi Julai 20, mwaka huu huku wakiendelea kunyimwa dhamana na kurudishwa rumande katika gereza la Keko.
  Wawili hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 29, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Victoria Nongwa kwa makosa matano wanayodaiwa kuyafanya kwa nyakati tofauti yakiwemo ya utakatishaji fedha ambayo hayana dhamana.
  Miongoni mwa mashtaka yanayowakabili ni pamoja na kughushi nyaraka zinazodaiwa kuwa klabu ya Simba inawalipa madeni watuhumiwa hao kiasi cha dola za Kimarekani 300,000 (Zaidi ya shilingi milioni 700 za kitanzania).
  Makosa mengine ni Aveva kutoa nyaraka za uongo kwa Benki ya CRDB Tawi la Azikiwe Dar es Salaam Machi 10, 2016, la tatu ni kutakatisha fedha kinyume cha sheria, ambapo inadaiwa rais huyo na Kaburu walikula njama za kufanya uhalifu huo.
  Shitaka la nne ni Kaburu kutakatisha fedha dola 300,000 na kuziweka katika Benki ya  Barclays Tawi la Mikocheni mjini Dar es Salaam, na la tano ni kutakatisha fedha  likimhusu tena, Makamu wa Rais, Kaburu anayedaiwa kumsadia Aveva kutakatisha fedha katika benki ya Barclays baada ya kughushi nyaraka.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: MHADHIRI VYUO VYA ULAYA AWA KATIBU MKUU SIMBA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top