• HABARI MPYA

    Friday, July 14, 2017

    MBAO FC: TUNAJIUMBA UPYA, MTATUTAMANI TENA MSIMU UJAO

    Na Mwandishi Wetu, MWANZA
    MWENYEKITI wa Mbao FC, Solly Zephania Njashi amewaondoa hofu wana Mwanza juu ya timu hiyo kuondokewa na wachezaji wengi nyota, akisema kwamba wanaisuka upya na itaendelea kutisha msimu ujao. 
    Katika mahojiano maalum na Bin Zubeiry Sports – Online jana, Njashi alisema kwamba uongozi upo bega kwa bega na benchi la Ufundi katika kuhakikisha wanasajiliwa wachezaji wengine wazuri kuziba mapengo ya walioondoka.
    Kauli huyo ya Mwenyekiti, inafuatia Mbao FC kuondokewa na wachezaji watano nyota baada ya msimu, ambao ni kipa Benedict Haule, kiungo Salmin Hoza waliokwenda Azam FC, kipa Emmanuel Mseja, beki Jamal Mwambeleko waliokwenda Simba na kiungo Pius Buswita aliyejiunga na Yanga. 
    Toa wanne; Wachezaji wanne hapa kipa Benedict Haule, beki Jamal Mwambeleko na viungo Salmin Hoza na Pius Busitwa pamoja na kipa wa akiba Emmanuel Mseja wameondoka

    “Ni kweli hao vijana wameondoka na walikuwa wachezaji wetu wa kikosi cha kwanza msimu uliopita, lakini ninataka nikuhakikishie Mbao inasukwa upya na itarudi na makali kuliko ya msimu uliopita,”alisema Njashi.
    Mwenyekiti huyo wa washindi wa pili wa Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC), Mbao FC ya Mwanza amesema kikubwa anachofurahi ni kocha wao, Mrundi, Etienne Ndayiragije kukubali kuendelea kuifundisha timu hiyo licha ya tetesi za kuhamia Simba.
    “Napenda pia ukanushe huu uvumi eti kocha wetu anaondoka. Hapana, kocha yupo na anaendelea na kazi na hivi yupo katika harakati za kujenga timu imara zaidi ya msimu ujao,”amesema Njashi.
    Pamoja na kupanda Ligi Kuu ‘kimazabe’ kufuatia kuenguliwa kwa Geita Gold iliyokutwa na hatia ya kupanga matokeo, lakini Mbao FC ilionyesha upinzani katika Ligi Kuu na kukaribia kutwaa Kombe la ASFC, ikiwatoa waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga katika Nusu Fainali kabla ya kufungwa kwa mbinde na Simba katika fainali mjini Dodoma.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MBAO FC: TUNAJIUMBA UPYA, MTATUTAMANI TENA MSIMU UJAO Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top