• HABARI MPYA

  Wednesday, July 05, 2017

  KILA LA HERI TAIFA STARS, CHIPOLOPOLO KITU GANI!

  Na Mwandishi Wetu, RUSTERNBURG
  TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars leo inateremka kwenye Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini kumenyana na Zambia katika Nusu Fainali ya Kombe la COSAFA Castle.
  Zambia, Chipolopolo imefika Nusu Fainali baada ya kuitoa Botswana kwa kuifunga 2-1 Jumamosi, wakati Tanzania iliwatoa wenyeji Afrika Kusini kwa kuwachapa 1-0. 
  Zambia na Tanzania zinakutana tena baada ya miaka mitatu, kufuatia mara ya mwisho kukutana Desemba 12, mwaka 2013 katika mchezo wa kuwania nafasi ya tatu, Kombe la CECAFA Challenge nchini Kenya na baada ya sare ya 1-1 ndania ya dakika 120, Chipolopolo wakashinda kwa penalti.
  Na kwa ujumla, kabla ya leo, timu hizo zimekwishakutana mara 30, Tanzania ikishinda mechi tano na Zambia ikishinda mechi 16, huku mechi tisa zikiisha kwa sare. Julai 5 kama leo, mwaka 1997 zilikutana katika Kombe la COSAFA pia na na zikamalizana kwa sare ya 2-2, lakini leo lazima mshindi apatikane.
  Tanzania ilianzia hatua ya mchujo kwenye Kundi A ambako iliongoza kwa pointi zake tano sawa na Angola baada ya sare mbili 0-0 na Angola, 1-1 na Mauritius na ushindi wa 2-0 dhidi ya Malawi, hivyo kutengeneza wastani mzuri wa mabao na kuwapiku wapinzani kusonga Nusu Fainali.
  Zambia yenyewe ilianzia moja kwa moja hatua ya Robo Fainali sawa na Afrika Kusini, Botswana, 
  Namibia, Lesotho na Swaziland huku Zimbabwe ikiongoza Kundi B. Lesotho na Zimbabwe zitamenyana katika Nusu Fainali ya pili Saa 2:00 usiku.
  Beki Abdi Hassan Banda anatarajiwa kurejea kwenye kikosi cha kwanza cha Taifa Stars leo baada ya kumaliza kutumikia adhabu ya kadi, lakini kocha Salum Mayanga anaweza kuwakosa majeruhi beki Shomary Kapombe na kiungo Raphael Daudi walioumia kwenye mchezo wa Nusu Fainali dhidi ya Afrika Kusini.
  Ikumbukwe, Mayanga ataendelea kumkosa mshambuliaji Mbaraka Yussuf Abeid aliyeathiriwa na hali ya hewa ya baridi, maana yake leo anaweza kuendelea kuwaanzisha pamoja Elias Maguri na Thomas Ulimwengu.  
  Bila shaka ukuta wa Stars utaendelea kuundwa na ‘TZ One’, Aishi Manula, Gardiel Michael, Salim Mbonde na Banda huku ukiwepo uwezekano mkubwa wa Hassan Kessy kuchukua nafasi ya Kapombe leo.
  Hapana shaka Mayanga ataendelea kulundika viungo wengi katikati wakiongozwa na Nahodha Himid Mao, Muzamil Yassin, Erasto Nyoni huku akitumia winga mmoja, Shiza Kichuya na Simon Msuva tumtarajie kipindi cha pili kama kawaida.
  Mchezo huo unaoatarajiwa kuanza Saa 12:00 jioni, unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua kama ilivyo kawaida ya zinapokutana Chipolopolo na Taifa Stars. Kila la heri Taifa Stars. Mungu ibariki Tanzania. Amin. 
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KILA LA HERI TAIFA STARS, CHIPOLOPOLO KITU GANI! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top