• HABARI MPYA

  Saturday, July 08, 2017

  KARIA AWAPONGEZA TAIFA STARS KWA USHINDI WA TATU COSAFA

  Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
  KAIMU Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, ameipongeza Taifa Stars kwa mafanikio ya kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Castle la Cosafa - inayoandaliwa na Baraza la Soka kwa nchi za Kusini mwa Afrika.
  “Haya ni matunda ambayo tunayaota kila wakati kwa timu kupata ushindi. Tunawapongeza wachezaji, benchi nzima la ufundi likiongozwa na Kocha Salum Mayanga, pamoja na watendaji wote kwa mafanikio ya timu yetu ya Taifa Stars,” amesema Karia.
  Amesema kwamba timu hiyo imeonyesha uzalendo wa hali ya juu katika kutafuta mafanikio na ana imani kwamba Tanzania itashiriki michuano mingi ya kimataifa kwa kuwa ina wachezaji wengi makinda huku TFF ikiendelea kuwakuza wengine kwa ajili ya kutimiza ndoto za furaha ya Watanzania kwa sasa na hapo baadaye.
  Taifa Stars jana usiku Julai 7, mwaka huu iliifunga Lesotho katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu wa michuano ya Castle Cosafa kwa mapigo 4-2 ya penalti katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Moruleng nchini Afrika Kusini.
  Katika mchezo huo wa jana, mabao ya Taifa Stars jana yalifungwa na Himid Mao, Abdi Banda, Simon Msuva na Raphael Alpha. Taifa Stars walikosa mkwaju mmoja wa penalti uliopigwa na Shiza Kichuya kwa kugongesga mwamba wa juu, lakini Lesotho walikosa mapigo mawili - moja likiwa limegonga mwamba wa pembeni na jingine likipanguliwa na Kipa Said Mohammed.
  Taifa Stars inatarajiwa kurejea usiku wa kuamkia kesho Jumapili Julai 9, mwaka huu saa 9.30 usiku kwa ndege ya Shirika la Ndege la Rwanda ambako itajipanga kwenda Mwanza siku ya Jumatatu saa 12.00 jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege la Fast Jet.
  Itakwenda Mwanza kujiandaa na mchezo dhidi ya Rwanda unaotarajiwa kufanyika Jumamosi Julai 15, mwaka huu katika mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).
  Timu hiyo ambayo kwa mwaka huu imecheza mechi tisa za kimataifa na kushinda mitano; kutoka sare miwili na kufungwa mmoja wa nusu fainali za Cosafa, itakuwa na kikosi cha wachezaji 20.
  Wachezaji wanne hawatakuwako kwenye kikosi ambao ni majeruhi Mbaraka Yussuf na Shaban Idd Chilunda kadhalika nyota wa kimataifa ambao hawahusiki na mechi za CHAN ambao ni Thomas Ulimwengu na Elius Maguri.
  Tayari Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amewaongeza nyota wawili katika kikosi hicho ambao ni John Bocco na Kelvin Sabato kutoka Majimaji ya Songea kujaza nafasi za Chilunda na Mbaraka.
  Pia amemwita  kinda Athanas Mdamu ambaye ni mchezaji mwanafunzi kutoka Shule ya kukuza vipaji ya Alliance ya Mwanza ili kumpatia uzoefu kwenye timu ya taifa ya wakubwa. Mdamu ataungana na timu huko Mwanza yaliko makazi yake.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: KARIA AWAPONGEZA TAIFA STARS KWA USHINDI WA TATU COSAFA Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top