• HABARI MPYA

    Tuesday, July 04, 2017

    KAMATI YA UCHAGUZI YAUNDWA UPYA, MCHAKATO KUENDELEA BILA MALINZI

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imefanya mabadiliko ya Kamati ya Uchaguzi na kuwaengua Wajumbe wanne walioonyesha kumtetea Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi ambaye kwa sasa yuko rumande kwa tuhuma mbalimbali.
    Uamuzi huo umefikiwa baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika leo mchana makao makuu ya shirikisho hilo, Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam chini ya Kaimu Rais, Wallace Karia.
    Wajumbe walioondolewa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Wakili Domina Madeli, Juma Lallika, Jeremiah Wambura na Hamim Mahmoud Omar na sasa Mwenyekiti, Wakili Revocatus Kuuli atafanya kazi na Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa, Wakili Malangwe Ally Mchungahela, Wakili Kiomoni Kibamba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza ma Wakili Thadeus Kalua.
    Kabla ya hapo, Mwenyekiti Kuuli alitofautiana na Wajumbe wenzake wote wa Kamati hiyo ya awali juu ya Malinzi kuruhusiwa kuendelea kuogombea katika uchaguzi wa Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma licha ya kwamba hakutokea kwenye usajili.
    Mchakato wa uchaguzi wa TFF sasa utaendelea bila Jamal Malinzi (katikati)
    Malinzi hakutokea kwenye usaili kutokana na kuwa anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kabla ya kufikishwa Mahakamani kusomewa mashitaka 28, ambayo yalimfanya anyimwe dhamana na kupelekwa rumande hadi Julai 17, mwaka huu upelelezi wa kesi uyake utakapokamilika.
    Wakili Kuuli alipingana na wenzake waliotaka Malinzi aruhusiwe kuendelea na mchakato japo hakushiriki usaili na kufikia kuvunja kikao, kisha kupeleka taarifa Kamati ya Utendaji ya TFF, ambayo nayo baada ya kikao chake cha leo imefikia uamuzi wa kuiunda upya Kamati ya uchaguzi pamoja na Kamati nyingine. 
    Kamati nyingine zilizotajwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi leo ni Kamati Maadili ambayo inaindwa na Mwenuekiti, Amidou Mbwezeleni, Steven Zangira, Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Glorius Luoga, Walter Lungu na Amin Bakhresa.
    Kamati ya Rufaa ya Maadili; Wakili Rugemeleza Nshala, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohammed Mpinga, Wakili Benjamin Karume, Dk Lisobine Chisongo, ASP Benedict Nyagabona.
    Kamati ya Nidhamu; Tarimba Abbas, Peter Hela, Boniface Lyamwike, Dk Billy Aonga na Kassim Dau, Kamati ya Rufaa ya Nidhamu; Wakili Rahim Zubeiry Shaaban, Siza Chenga, Abbas Mtemvu, Amani Mulika na Stella Mwakingwe wakati Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi inaundwa na Wakili Abdi Kagomba, Kenneth Mwenda, Rashid Sadallah, Jabir Shekimweri na Mohamed Gombati.
    Sasa Kamati mpya ya Uchaguzi inatarajiwa kuendelea na mchakato, ambao ulisimamishwa kwa muda Julai 2 ukiwa katika hatua ya usaili.
    Malinzi, Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa kwa pamoja na Mhasibu, Nsiande Isawafo Mwanga wako kwa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam na wanatarajiwa kufikishwa tena Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam Julai 17, mwaka huu.
    Wakati huo huo: Ujumbe wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hautakuja tena nchini baada ya mazungumzo na Kaimu Rais wa TFF, Wallace Karia kwa njia nya simu.
    Karia amesema katika mazungumzo hayo amewaeleza kila kitu kinachoendelea nchini ikiwemo kikao cha leo cha Kamati ya Utendaji na wameridhika na kuitakia kila la heri kamati hiyo.
    “FIFA hawatakuja tena, tuliongea nao tukawaeleza kinachoendelea, walitupigia wakitaka kujua kama kulikuwa na muingilio wa serikali katika mchakato, au kama kuna fedha za FIFA zilizotumika vibaya, tukawaambia siyo kweli na kuwaeleza kilichotokea kwa hiyo hawatakuja,” amesema Karia.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KAMATI YA UCHAGUZI YAUNDWA UPYA, MCHAKATO KUENDELEA BILA MALINZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top