• HABARI MPYA

    Wednesday, July 05, 2017

    HAJIB APEWA JEZI YA TEGETE YANGA

    Na Mwandishi Wetu, DAR ES SALAAM
    YANGA SC imemkabidhi jezi namba 10 mshambuliaji wake mpya, Ibrahim Hajib Migomba iliyemsajili kutoka kwa mahasimu, Simba SC.
    Katika mkutano maalum wa kumtambulisha mchezaji huyo mjuzi wa kiwango cha juu kwa uchezaji mpira wa miguu, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh amemkabidhi jezi namba 10, iliyokuwa inavaliwa na mkali wa mabao wa timu hiyo, Jerson John Tegete.
    Jezi namba 10 haikuwahi kupata mtu wa ‘kuitendea haki’ Jangwani tangu kuondoka kwa Tegete na miongoni na mtu wa mwisho kuivaa ni Matheo Anthony Simon, ambaye anaachwa baada ya kumaliza mkataba wake. 
    Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh (kushoto) akimkabidhi jezi namba 10 mshambuliaji mpya, Ibrahim Hajib (kulia)


    Ibrahim Hajib akiwa na Katibu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa

    Hajib alikabidhiwa jezi hiyo baada ya kukamilisha usajili wake makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam leo

    Hajib ni mchezaji aliyeibukia timu ya vijana ya Simba, ambayo ilimtoa Boom FC ya Ilala mwaka 2013, lakini baadaye akaondoka kwenda kujikomaza kwenye timu ambazo angepata nafasi ya kucheza. 
    Alichezea Mwadui FC na kuisaida kupanda Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2014-2015 kabla ya kurejeshwa Msimbazi.
    Alikuwa na mwanzo mzuri Simba SC chini ya kocha Mserbia, Goran Kopunovic na nyota yake kidogo iliendelea kung’ara chini ya kocha Muingereza, Dylan Kerr ingawa baada ya ujio wa Mganda Jackson Mayanja na baadaye Mcameroon, Joseph Marius Omog mambo yakaanza kuwa tofauti kidogo.
    Habari za Hajib kuondoka Simba zilitarajiwa, kwani mchezaji huyo amekuwa hana furaha katika klabu hiyo kutokana naa kile kilichoonekana kama kutokubalika mbele ya viongozi wengi wa klabu hiyo.
    Jerry Tegete ni mchezaji wa mwisho kufanya vizuri Yanga akiwa na jezi namba 10
    Matheo Anthony alipewa jezi namba 10 mwaka juzi baada ya kusajiliwa kutoka KMKM, lakini ameshindwa kuitendea haki

    Walikuwa wanamchukulia kama mchezaji asiye na faida kikosini pamoja na kukiri juu ya uwezo wake mkubwa kisoka, jambo ambalo lilimfanya muda mrefu wa msimu awe anawekwa benchi.
    Na Hajib mwenyewe mapema tu alionyesha nia ya kuondoka Msimbazi ingawa mpango wake wa awali ulikuwa ni kwenda nje.
    Mwanzoni mwa msimu uliopita alikwenda Afrika Kusini kwa majaribio ambako iliripotiwa alifuzu klabu ya Lamontville Golden Arrows FC ya Ligi Kuu ya ABSA, lakini mkataba wake na Simba ukamzuia kuondoka.
    Na katikati ya msimu uliopita pia, Hajib alikwenda Haras El Hodoud ya Misri ambako iliripotiwa pia amefuzu na atajiunga na klabu hiyo akimaliza mkataba wake Simba, lakini sasa anaibukia Yanga.
    Hajib anakuwa mchezaji wa tatu mpya kusajiliwa Yanga, baada ya beki Abdallah Hajji Shaibu ‘Ninja’ kutoka Taifa Jang’ombe ya Zanzibar na kiungo Pius Buswita kutoka Mbao FC ya Mwanza.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HAJIB APEWA JEZI YA TEGETE YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top