• HABARI MPYA

    Wednesday, July 12, 2017

    ‘FUNDI KIRAKA’ ERASTO EDWARD NYONI ANATUA YANGA

    Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
    KIUNGO anayeweza kucheza nafasi zote za ulinzi, Erasto Edward Nyoni yuko mbioni kujiunga na mabingwa wa Tanzania, Yanga baada ya kumaliza mkataba wake Azam FC.
    Nyoni yupo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayojiandaa kwa mchezo na Rwanda Jumamosi Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), michuano inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee – na Yanga wanatarajia kumalizana naye kabisa baada ya mechi hiyo.
    “Mazungumzo na Nyoni yamekwenda vizuri na wakati wowote tunaweza kumalizana naye, pengine baada ya mechi tu dhidi ya Rwanda,”kimesema chanzo kutoka Yanga.
    Mkongwe Erasto Nyoni akimburuza mchezaji wa Mauritius katika mechi ya Kombe la COSAFA mapema mwezi huu mjini Rusternburg, Afrika Kusini

    Benchi la Ufundi la Yanga, chini ya Kocha Mkuu, Mzambia George Lwandamina kwa kushirikiana na Sekretarieti chini ya Katibu Mkuu, Charles Boniface Mkwasa ambaye kitaaluma ni kocha kwa pamoja wamejiridhisha Nyoni ni mchezaji ambaye wanamuhitaji kikosini.
    Na hiyo ni kwa sababu huyo ni ‘kiraka’ anayeweza kucheza nafasi yoyote ya ulinzi kuanzia kiungo wa ulinzi – lakini uzoefu na weledi wake kisoka ni vitu vingine vinavyomuunganisha na Yanga katika siku za mwishoni za maisha yake ya uwanjani.  
    Erasto ni mchezaji pekee ambaye alikuwepo timu ya taifa kanzia wakati wa Mbrazil, Marcio Maximo mwaka 2006 na ameendelea kuitwa na kila kocha aliyefuatia kupewa jukumu la kuifundisha timu hiyo kuanzia Wadenmark Jan Borge Poulsen, Kim Poulsen, Mholanzi, Mart Nooij na wazalendo Mkwasa na huyu wa sasa, Salum Mayanga.
    Pamoja na kucheza nafasi za ulinzi, lakini Nyoni ameifungia Stars mabao manne ya kukumbukwa, likiwemo bao pekee katika ushindi wa 1-0 ugenini dhidi ya wenyeji Burkina Faso, Juni 16, mwaka 2007 mjini Ouagadougou katika mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2010.
    Na hilo ndilo lilikuwa bao lake la kwanza Taifa Sars kabla ya kufunga tena Juni 10, mwaka 2012 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao la ushindi, Tanzania ikiilaza 2-1 Gambia katika mechi ya kufuzu Kombe la Dunia.
    Akafunga bao la kwanza katika sare ya 3-3 na wenyeji Botswana Uwanja wa Molepolole mjini Molepolole, Agosti 15, 2012 kwenye mchezo wa kirafiki, kabla ya Julai 5, mwaka huu kufunga bao la kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la COSAFA Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini Taifa Stars ikifungwa 4-2 na Zambia waliotoka nyuma kwa 1-0.
    Nyoni ambaye Mei 7, mwaka huu amefikisha miaka 29, amekuwa mchezaji wa Azam FC tangu mwaka 2010 alipojiunga nayo kutoka Vital’O ya Burundi iliyomchukua AFC ya Arusha alikocheza kidogo tu akitokea kituo cha Rollingston cha mjini humo.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ‘FUNDI KIRAKA’ ERASTO EDWARD NYONI ANATUA YANGA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top