• HABARI MPYA

  Monday, July 10, 2017

  BANDA ALALAMIKA SIMBA WANATAKA KUMPEPERUSHIA ‘ZALI’ LAKE LA SAUZI

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Hassan Banda amelalamika klabu ya Simba inataka kukwamisha mpango wake wa kujiunga na klabu ya Baroka F.C ya Afrika Kusini.
  Banda amesaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga na Baroka ya Ligi Kuu wiki iliyopita baada ya kung’ara katika michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini akiiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu.
  Lakini baada ya kurejea nyumbani jana kushughulikia vibali na kukamilisha taratibu mbalimbali za uhamisho wake, amekutana na vikwazo.
  Abdi Banda (kushoto) amesajiliwa na Baroka F.C. ya Afrika Kusini baada ya kung'ara kwenye michuano ya COSAFA

  “Mimi nimemaliza mkataba wangu Simba. Sasa nimekuja kufuata barua ya uthibitisho kwamba mimi si mchezaji wa Simba tena, lakini wananipiga chenga kuniandikia, hili jambo si zuri na isitoshe muda nilionao ni mchache sana kukamilisha hizi taratibu,”amesema Banda akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online jioni hii.
  Banda amesema amefika makao makuu ya klabu, Msimbazi, Dar es Salaam tangu Saa 4:05 asubuhi, lakini hadi Saa 11:00 jioni hakubahatika kupata barua hiyo kutokana na chenga alizopigwa na Kaimu Katibu Mkuu, Hamisi Kisiwa.
  “Kwa kweli inaumiza sana, nimeitumikia hii klabu vizuri tu kwa moyo wangu wote katika kipindi chote cha miaka miwili, haipendezi kuachana nayo vibaya, ikiwa mimi mwenyewe nimetumia njia za kiungwana sana,”amesema Banda. 
  Banda amesema kwamba anatakiwa kurejea haraka Afrika Kusini kupeleka vielelezo alivyoagizwa na timu hiyo ya Ga-Mphahlele, karibu na Polokwane, Limpopo ikiwemo barua ya uthibitisho wa kumaliza mkataba, lakini ajabu Simba wanamkwamisha.
  Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Salim Abdallah, Kaimu Makamu Mwenyekiti, Iddi Kajuna na Kisiwa wote hawakupatikana walipotafutwa jioni ya leo kuzungumzia hilo.
  Banda alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza michuano ya COSAFA Castle na kutwaa Medali ya Shaba baada ya ushindi wa penalti 4-2 Ijumaa dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa jana Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, tena akipiga moja ya matuta hayo manne.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BANDA ALALAMIKA SIMBA WANATAKA KUMPEPERUSHIA ‘ZALI’ LAKE LA SAUZI Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top