• HABARI MPYA

  Saturday, July 08, 2017

  BANDA AAGA RASMI SIMBA, ASAINI MIAKA MITATU SAUZI

  Na Rehema Lucas, DAR ES SALAAM
  BEKI wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Hassan Banda amefikia makubaliano na klabu ya Baroka F.C ya Afrika Kusini kusaini mkataba wa miaka mitatu kujiunga nayo.
  Baada ya kung’ara katika michuano ya Kombe la COSAFA Castle nchini Afrika Kusini akiiwezesha Tanzania kushika nafasi ya tatu, mchezaji huyo wa Simba ya nyumbani, Tanzania sasa anakaribia kwenda kuanza maisha mapya timu hiyo ya Ga-Mphahlele, karibu na Polokwane, Limpopo ambayo inacheza Ligi Kuu ya nchini humo.
  Banda amesema anaondoka Simba SC aliyoichezea kwa miaka miwili, baada ya kumaliza mkataba wake na hakuwahi kusaini mkataba mpya, hivyo anajiunga na Baroka kama mchezani huru.
  Abdi Banda amefikia makubaliano na Baroka F.C ya Afrika Kusini kusaini mkataba wa miaka mitatu

  “Nipo njiani narudi nyumbani kwa ajili ya kuja kuchukua vitu na kurudi rasmi Afrika Kusini kuanza maisha mapya na klabu yangu mpya ya Baroka,”amesema Banda akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online kwa simu leo.
  Banda alikuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kilichocheza michuano ya COSAFA Castle na kutwaa Medali ya Shaba baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa jana Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg.
  Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao, Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.
  Kipa wa Tanzania, Said Mohammed Mduda alipangua ya nne ya Lesotho iliyopigwa na Nahodha wao, Thapelo Mokhehle kufuatia Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani. Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle.
  Kutoka na ushindi huo, Tanzania inaondoka na dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300.
  Fainali ya COSAFA Castle 2017 itachezwa Jumapili Uwanja wa Royal Bafokeng, Phokeng mjini Rusternburg baina ya majirani, Zambia na Zimbabwe na bingwa atapata dola 42,000 na mshindi wa pili dola 21,000.
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: BANDA AAGA RASMI SIMBA, ASAINI MIAKA MITATU SAUZI Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top