• HABARI MPYA

    Thursday, June 08, 2017

    YANGA NAYO YATUPWA NJE MICHUANO YA SPORTPESA

    Na Shekha Jamal, DAR ES SALAAM
    MABINGWA wa Tanzania, Yanga wamekuwa timu ya mwisho ya nyumbani kuaga michuano ya SportPesa Super Cup baada ya kutolewa kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 mchana wa leo Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
    Kwa matokeo hayo, Leopards itamenyana na mshindi kati ya Gor Mahia na Nakuru All Stars zote Kenya katika Fainali Jumapili na mshindi atajinyakulia dola za kimarekani 30,000 zaidi ya Sh. Milioni 65 na nafasi ya kucheza na Everton ya England Julai 13.  
    Kipa namba moja wa Yanga, Deogratius Munishi ‘Dida’ aliokoa mkwaju wa Marselas Ingotsi, lakini mlinda mlango wa AFC Leopards, Dennis Shikai naye akacheza mikwaju ya Said Mussa na Said Juma ‘Makapu’.
    Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi aliyeiongoza timu kwenye michuano ya SportPesa Super Cup kutokana na bosi wake, Mzambia George Lwandamina kuwa kwao likizo akifuatilia mchezo dhidi ya AFC Leopards leo
    Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Juma Mahadhi akimuacha chini beki wa Tusker FC

    Kiungo wa Yanga, Yussuf Mhilu (kushoto) akimpita beki wa AFC Leopards, Marcus Abwao

    Beki wa Yanga, Juma Abdul akinyoosha mguu juu kuokoa dhidi ya mchezaji wa Leopards

    Obrey Chirwa wa Yanga akipiga shuti katikati ya wachezaji wa AFC Leopards
    Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kiungo mshambuliaji Mzambia, Obrey Chira ndiyo pekee walifunga penalti za Yanga, wakati Bernard Mango, Allan Katerega, Duncan Otieno na Dennis Shikai wakafunga za AFC Leopards.
    Katika dakika 90 za kawaida za mchezo, timu zote zilimiliki mpira sawa, ingawa hakukuwa na mashambulizi ya kushitua.
    Allan Kateregga wa AFC Leopards alipiga shuti kali dakika ya 39, lakini kipa wa Yanga, Dida akadaka. Kiungo chipukizi wa Yanga, Yussuf Mhilu alipiga shuti zuri dakika ya 43, lakini beki wa AFC Leopards, Joshua Mawira akaokoa.
    AFC Leopards wakapoteza nafasi nyingine baada ya Vincent Oburu kushindwa kutumia pasi ya Ingotsi kwa kupiga shuti dhaifu lililodakwa na Dida. Chirwa naye akapiga krosi nzuri dakika ya 60, lakini mpira ukatoka nje.
    Chipukizi Maka Edward Mwakalukwa naye akapiga nje dakika ya 62 baada ya kupokea pasi ya Juma Mahadhi.
    Kikosi cha Yanga kilikuwa: Deogratius Munishi ‘Dida’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul, Mohammed Ally, Andrew Vincent ‘Dante’, Pato Ngonyani/Babu Ally Seif dk61, Juma Mahadhi, Maka Edward/Said Juma dk76, Obrey Chirwa, Yussuf Mhilu/Samuel Greyson dk53 na Emmanuel Martin/Said Mussa dk56.
    AFC Leopards: Dennis Shikai, Otieno Ian, Marcus Abwao/Mike Kibwage dk88, Joshua Mawira, Salim Abdallah, Duncan Otieno, Mango Bernard, Allan Kateregga, Vincent Obura, Yakubu Ramadhani na Gilbert Fiamento/Marselas Ingotsi dk56.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA NAYO YATUPWA NJE MICHUANO YA SPORTPESA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top