• HABARI MPYA

  Sunday, June 11, 2017

  VITA YA MASHEMEJI LEO SHAMBA LA BIBI, YETU MACHO!

  Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
  KAPETI la nyasi za bandia za Uwanja wa Uhuru leo litatimbika kwa mchezo wa fainali ya michuano mipya kabisa, SportPesa Super Cup baina ya mahasimu wa Kenya, Gor Mahia na AFC Leopards.
  Mchezo huo maarufu kama ‘Derby ya Mashemeji’ unatarajiwa kuanza Saa 10:00 jioni na bingwa atajinyakulia kitita cha dola za Kimarekani 30,000 na nafasi ya kucheza na Everton ya England Julai 13, Uwanja wa Taifa,, Dar es Salaam. 
  Leopards maarufu kama Ingwe iliingia fainali baada ya kuwatoa mabingwa wa Tanzania, Yanga kwa penalti 4-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika ya 90 na Gor Mahia kuifunga 2-0 Nakuru All Stars ya Kenya pia.
  Nyomi; Hivi ndivyo Uwanja huwa unafurika Mashemeji wanapomenyana nyumbani. Leo itakuwaje Dar es Salam?

  Mamia ya mashabiki wa timu hizo zenye mvuto wa kipekee Kenya tayari wapo Dar es Salaam kutoka sehemu mbalimbali nchini humo ili kushuhudia fainali hiyo tamu na ya kihistoria Jumapili Uwanja wa Uhuru.
  Na kwa hapa nyumbani, tayari mashabiki wa timu pinzani za hapa wamegawana timu za kusapoti Jumapili, Yanga wakiichagua Gor Mahia inayotumia jezi za kijani na Simba wakiichagua Leopards (Chui) inayotumia jina la mnyama kama wao, lakini pia inavaa jezi nyekundu.
  Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Kenya Jumapili ya Mei 7, mwaka huu Uwanja wa Nyayo mjini Nairobi, Kenya.
  Na siku hiyo, Gor Mahia wakaibuka washindi wa ‘Derby’ ya kwanza ya msimu ya Mashemeji kwa kuilaza AFC Leopards 3-0, mabao ya Meddie Kagere dakika ya 18, George ‘Blackberry’ Odhiambo dakika ya 35 na Timothy Otieno dakika ya 83.
  Kagere, mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Rwanda mwenye asili ya Uganda, ndiye anaongoza kwa mabao katika michuano hii hadi sasa, akiwa amefunga mara tatu.
  Gor inaonekana kuwa katika kiwango bora zaidi kuelekea mchezo wa leo, kwani mechi zake zote mbili za awali imeshinda ndani ya dakika 90, awali ikiwafunga Jang’ombe Boys 2-0 pia, wakati Leopards hata mechi ya kwanza walifuzu kwa matuta pia wakiitoa Singida United kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 1-1.   
  Lakini matokeo au rekodi zozote za nyuma huwa hazina nafasi kwenye Mashemeji Derby, kwani timu hujipanga kivingine na huingia kitofauti kwa ajili ya mchezo husika. Ndiyo maana huu si mchezo wa kukosa, yafaa kwenda kujionea moto wa Mashemeji.  
  Loading...
  • Blogger Comments
  • Facebook Comments

  0 comments:

  Item Reviewed: VITA YA MASHEMEJI LEO SHAMBA LA BIBI, YETU MACHO! Rating: 5 Reviewed By: Bin Zubeiry Sports - Online

  PATA HABARI POPOTE ULIPO. ZIKITUFIKIA ZITAKUFIKIA

  Scroll to Top